RAIS MAGUFULI AMEKUTANA NA WATANZANIA WAISHIO NCHINI UGANDA
Na.Issack Gerald
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.John Pombe
Magufuli amekutana na Watanzania waishio nchini Uganda katika Mji wa Masaka na
kuwahakikishia kuwa hatua zilizoanza kuchukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano
katika kuleta mabadiliko zimeanza kuzaa matunda.
Mhe. Rais Magufuli aliyeongozana na Mkewe Mama Janeth
Magufuli, Mawaziri na viongozi wakuu wa taasisi za Serikali ametaja baadhi ya
matokeo hayo kuwa ni kusimamia vizuri uchumi unaokuwa kwa wastani wa asilimia
7, kudhibiti mfumuko wa bei hadi asilimia 5.1, kuokoa Shilingi Bilioni 238
walizokuwa wanalipwa watumishi hewa kwa mwaka na kuondoa watumishi wenye vyeti
feki waliokuwa wakilipwa Shilingi Bilioni 142 kwa mwaka.
Matokeo mengine ni kuongeza ukusanyaji wa mapato kutoka
Shilingi Bilioni 850 hadi wastani wa Shilingi Trilioni 1.2 kupitia Mamlaka ya
Mapato (TRA), kuanza ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard
Gauge) kuanzia Dar es Salaam hadi Dodoma umbali wa kilometa 726 ambapo
Shilingi Trilioni 7 zitatumika, kununua ndege 6 za Serikali kwa ajili ya kuinua
utalii na kuimarisha usafiri wa anga, kutoa elimu bila malipo kwa shule za
msingi na sekondari na kuboresha huduma za afya ikiwemo kuongeza bajeti ya dawa
kutoka Shilingi Bilioni 31 hadi 269.
Mhe. Rais Magufuli pia amesema Serikali imechukua hatua madhubuti
za kuwavutia wawekezaji na sasa wengi wapo katika hatua mbalimbali za uwekezaji
ikiwemo ujenzi wa viwanda na ametoa wito kwa Watanzania hao kuendelea
kuwashawishi wawekezaji wengine kwenda kuwekeza nchini Tanzania kwa kuwa fursa
zipo nyingi.
Katika mkutano huo Watanzania waishio Uganda wamemshukuru na
kumpongeza Mhe. Rais Magufuli kwa juhudi mbalimbali anazozifanya na wameomba
Serikali iwajengee mazingira bora pale wanapowapeleka wawekezaji nchini
Tanzania.
Pamoja na Mhe. Rais Magufuli kuahidi kufanyia kazi maoni ya
Watanzania hao, Mawaziri waliokuwa wakijibu hoja mbalimbali zilizotolewa
wamewataka kutosita kuwasiliana nao pale wanapokuwa na jambo linalohitaji
majibu ya Serikali.
Huu ni mkutano wa kwanza wa Mhe. Rais Magufuli kukutana na
Watanzania waishio nje ya nchi (Diaspora), na Uganda kuna Watanzania
45,000 waishio nchini hapa.
Habari zaidi ni
P5TANZANIA LIMITED
Comments