MARAIS MAGUFULI NA MSEVEN WAMETOA MAAGIZO KWA MAWAZIRI WA NCHI ZOTE MBILI
Na.Issack
Gerald
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe.Yoweri
Kaguta Museveni wamewaagiza Mawaziri wa nchi hizi mbili kujadiliana juu ya
namna ya kuongeza biashara kati ya nchi hizi ili kupata manufaa makubwa zaidi
ya uhusiano na ushirikiano wa kidugu uliopo.
Viongozi hao wametoa kauli hiyo leo baada ya kufanya
mazungumzo rasmi na kisha kuzungumza na waandishi wa habari katika Ikulu ndogo
ya Masaka nchini Uganda ambako Mhe.Rais Magufuli ameendelea na ziara yake rasmi
ya kiserikali ya siku 3.
Mhe. Rais Magufuli amesema kwa muda mrefu biashara kati ya
Tanzania na Uganda imekuwa ni takribani shilingi Bilioni 200 kwa mwaka kiasi
ambacho ni kidogo mno ikilinganishwa na fursa zilizopo, uhusiano na ushirikiano
wa kidugu uliojengwa tangu enzi za Baba wa Taifa Hayati Mwl.Julius Kambarage
Nyerere.
Kuhusu hatua ambazo Tanzania imeanza kuchukua Mhe.Rais
Magufuli amesema pamoja kuanza ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard
Gauge) kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma umbali wa kilometa 726, Serikali
imekarabati reli iliyopo,pamoja na kivuko cha mabehewa ya treni cha Umoja
katika ziwa Victoria ili kuwezesha mizigo ya kutoka bandari ya Dar es Salaam
kufika Kampala kwa gharama nafuu na pia inaendelea kujenga na kuimarisha
barabara za mpakani.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari Mhe.Rais Magufuli
ameeleza kuwa Tanzania imejipanga kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano wake
na Uganda kwa kuhakikisha miradi mbalimbali inakwenda vizuri ikiwemo kituo cha
pamoja cha huduma za mpakani (One Stop Border Post – OSBP) na mradi wa
bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi bandari ya Tanga nchini
Tanzania.
Kwa upande wake Mhe. Rais Museveni amempongeza Mhe. Rais Magufuli
kwa juhudi kubwa anazozifanya kupambana na rushwa na kuimarisha uchumi, na
amemuagiza Waziri wake wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Monica Azuba Ntege
kuharakisha mchakato wa ujenzi wa kipande cha reli cha kilometa 11 kutoka
bandari ya Portbell hadi Kampala ili usafirishaji wa mizigo kwa njia ya reli
kutoka bandari Dar es Salaam uanze mara moja.
Mhe. Rais Museveni amesisitiza kukuzwa kwa biashara katika ya
Tanzania na Uganda hasa wakati huu ambapo Uganda inahitaji kununua gesi ya
Tanzania kwa ajili ya viwanda vyake vya mbolea na chuma na pia kurudisha
historia ambapo Uganda ilikuwa mnunuzi mkubwa wa bidhaa za Tanzania.
Kabla ya kuzungumza na waandishi wa habari Marais wote wawili
wameshuhudua utiaji saini wa makubaliano ya ushirikiano kati ya Shirika la Utangazaji
Tanzania (TBC) na Shirika la Utangazaji wa Uganda (UBC) na
makubaliano kati ya Jeshi la Polisi la Tanzania na Jeshi la Polisi la Uganda.
Mhe. Rais Magufuli atamaliza ziara yake rasmi ya siku 3 kesho
na kurejea nchini Tanzania.
Habari zaidi ni P5TANZANIA LIMITED
Comments