HALI YA TAHARUKI MKOANI RUKWA,JENEZA LENYE MWILI WA MAREHEMU LIMETELEKEZWA
Na.Issack Gerald
Hali ya taharuki na hofu imezuka
katika Kijiji cha Katani Kata ya Nkandasi wilayani Nkasi mkoani Rukwa na
kusababisha waombolezaji kutimua mbio na kuacha jeneza lenye mwili wa marehemu
baada ya mvua kubwa kuanza kunyesha na kubomoa nyumba za wakazi wa kijiji
hicho.
Mwenyekiti wa serikali ya kitongoji
cha Kaungo, Robert Kanoni, alisema tukio hilo lilitokea jana saa 6
mchana, wakiwa wanaelekea kufanya maziko ya marehemu Dismas Kanoni
aliyefariki jana baada ya kuugua siku chache zilizopita, ghafla ilianza
kunyesha mvua kubwa ikiambatana na radi na upepo mkali ulioezua baadhi ya
nyumba hali iliyosababisha baadhi ya waombolezaji kutimua mbio na kurejea
majumbani kutokana na hofu iliyoibuka kufuatia tukio hilo.
Baadhi ya wananchi walivumilia
nakurejea na jeneza lililokuwa na mwili wa marehemu nyumbani na kuahirisha
maziko kwa muda ili kupisha hali hiyo itulie na walikwenda kuzika baadaye
katika makaburi yaliyopo kijijini hapo.
Alisema tukio hilo limezua hisia za
kishirikina kwa wananchi wa kijiji hicho kwani miezi miwili iliyopita baba yake
na marehemu huyo alifariki baada ya kugongwa na gari la kampuni ya ujenzi wa
barabara na walipofanya maziko siku iliyofuata walikuta ngozi ya kondoo juu ya
kaburi la marehemu kitendo kilichowashangaza.
Kanoni alisema kutokana na mvua hiyo,
nyumba zipatazo 10 zimebomoka kabisa na zinatakiwa kujengwa upya huku makazi
licha ya kuwa wamepata hifadhi na misaada ya kibinadamu kwa wenzao.
Naye Peter Kalale, mkazi wa kijiji
hicho akizungumzia tukio hilo, alisema mara kwa mara kijiji hicho kimekuwa
kikikumbwa na dhoruba pindi mvua zinaponyesha kwa kuwa kimepitiwa na mkondo wa
upepo mkali ambao unasababisha hali hiyo.
Mwenyekiti wa kamati ya maafa ya
wilaya hiyo ambaye ni Mkuu wa wilaya hiyo, Said Mtanda, alithibitisha
kutokea kwa tukio hilo na kutoa wito kwa wananchi kujenga makazi bora kwani
miongoni mwa nyumba hizo zipo ambazo zimeezekwa kwa nyasi.
Alisema sera ya serikali ya awamu ya
tano ni kuwahimiza wananchi wajenge nyumba bora na za kisasa ili waepuke
majanga yanayotokana na tabianchi kwani bila kufanya hivyo, wananchi
wataendelea kupata hasara.
Habari
Zaidi NA P5TANZANIA LIMITED
Comments