RAIS MAGUFULI ATOA SIKU 14 KWA WAMILIKI WA VITUO VYA MAFUTA KUFUNGA MASHINE ZA KIELECTRONIKI ZA KUTOA RISITI-Julai 19,2017
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe
Magufuli ametoa siku 14 kwa wamiliki wa vituo vyote vya mafuta nchini kufunga
na kutumia mashine za kielektroniki za kutolea risiti (Electronic Fiscal Petrol Printer).
Mhe. Rais
Magufuli ametoa agizo hilo leo,wakati akizungumza na wananchi wilayani
Biharamulo Mkoani Kagera muda mfupi kabla ya kufungua barabara ya lami ya
Kagoma – Biharamulo – Lusahunga.
Aidha Mhe. Dkt.
Magufuli ameiagiza Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara ya Viwanda,Biashara na
Uwekezaji kuhakikisha vituo vyote vya mafuta nchini vinatumia mashine hizo na
kusisitiza kuwa wamiliki watakaokiuka agizo hilo vituo vyao vifungwe na
kufutiwa leseni.
Katika hatua
nyingine,Mhe.Rais Magufuli pia amewataka wafugaji waliovamia hifadhi ya Burigi
Mkoani Kagera kuondoa mifugo yao mara moja na amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Kagera
Meja Jenerali Mstaafu Salum Kijuu kuendelea na operesheni ya kuondoa mifugo
yote iliyovamia hifadhi hiyo na maeneo mengine yasiyoruhusiwa kupeleka mifugo.
Amewataka
wafugaji kote nchini kuchunga mifugo yao katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili
ya kulisha mifugo na ameonya kuwa vitendo vya wafugaji kuingiza mifugo yao
katika hifadhi na mashamba ya wakulima havikubaliki.
Kuhusu kero ya uhaba wa maji inayowakabili wananchi wa Biharamulo,Mhe.
Rais Magufuli ameelezea kusikitishwa na kasi ndogo ya utekelezaji wa mradi wa
kupeleka maji katika mji huo na amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji
safi na Maji Taka Bukoba (BUWASA) Alen Mwita
kuhakikisha mashine zilizonunuliwa zinafungwa na kuanza kutoa maji ifikapo
tarehe 30 Julai, 2017.
Baada ya
kuzungumza na wananchi wa Biharamulo katika mkutano wa hadhara uliofanyika
katika kituo cha mabasi, Mhe. Rais Magufuli amefungua barabara ya Kagoma –
Biharamulo – Lusahunga ambayo inaunganisha mawasiliano ya barabara kati ya
mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Kigoma, Shinyanga na nchi jirani za Burundi,
Rwanda na Uganda.
Barabara hiyo
ina urefu wa Kilometa 154 na imejengwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 190.4
zilizotolewa na Serikali ya Tanzania.
Mapema leo
asubuhi Mhe. Rais Magufuli ametembelea Seminari ya Mtakatifu Karoli Lwanga
Katoke alikosoma elimu ya sekondari ambapo ameendesha harambee iliyofanikisha
kupatikana mifuko 1,000 ya saruji na mabati 150 kwa ajili ya kuchangia ujenzi
wa majengo ya Seminari hiyo, na pia ametoa Shilingi Milioni 1 kwa ajili ya
kutengeneza dirisha la bweni alilolivunja wakati akiwa kidato cha pili pamoja
na madirisha mengine yanayohitaji matengenezo.
Akiwa njiani
kuelekea Ngara, Mhe. Rais Magufuli amesimamishwa na wananchi wa Nyakahura
ambapo amewahakikishia kuwa Serikali itaifanyia matengenezo barabara ya
Nyakahura – Rusumo – Ngara, ameahidi kumtuma Waziri wa Maji na Umwagiliaji
kwenda kuangalia namna ya kutatua tatizo la maji na pia amechangia Shilingi
Milioni 10 katika ujenzi wa majengo ya shule.
Kesho tarehe 20
Julai, 2017 Mhe. Rais Magufuli ataendelea na ziara yake Mkoani Kagera ambapo
hapa Ngara atazungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara utakaofanyika
mchana.
Bonyeza P5TANZANIA.BLOGSPOT.COM kwa habari zaidi
Comments