WAZIRI MKUU ATOA SIKU MBILI KWA MAOFISA ARDHI KUMALIZA KERO ZA WANANCHI


Na.Issack Gerald Bathromeo-Rukwa
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa siku mbili kwa Mkuu wa Idara ya Ardhi na Miundombinu wa mkoa wa Rukwa pamoja na Ofisa Ardhi wa Manispaa ya Sumbawanga kutatua matatizo ya ardhi yanayowakabili wakazi wa Manispaa hiyo.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa Mkoani Rukwa
                                                 

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana,wakati akizungumza na maelfu ya wakazi Mji wa Sumbawanga waliojitokeza katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kiwanja cha Mandela katika jimbo la Sumbawanga mjini aliwasisitiza watendaji hao kuwasikiliza wananchi na kutatua kero zao.
Alisema tangu alivyoanza ziara yake katika mikoa ya Rukwa na Katavi kila eneo alilopita amekutana na wananchi wakiwa na mabango yanaeleza changamoto na hii inatokana na viongozi wa mikoa hiyo kushindwa kutenga siku maalumu kwa ajili ya kusikiliza kero hizo.
Waziri Mkuu alibainisha kwamba baadhi ya mikoa na halmashauri mbalimbali nchini zimeshaanza utaratibu huo wa kutenga siku maalumu katika wiki na kusikiliza matatizo yanayowakabili wananchi jambo ambalo limeanza kuonesha mafanikio ya utatuzi wa kero hizo.
Awali akizungumza katika mkutano huo mbunge wa jimbo la Sumbawanga Mjini Aeshi Hilaly alisema wakazi wa Manispaa ya Sumbawanga wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya migogoro mikubwa ya ardhi, hivyo alimuomba Waziri Mkuu kuwasaidia katika kuipatia ufumbuzi.
Mbunge huyo alisema migogoro hiyo ambayo imedumu kwa muda mrefu imewasababishia usumbufu mkubwa wakazi wa jimbo hilo kukosa haki  zao na muda mwingi wamekuwa wakiutumia kufuatilia hatma ya ardhi yao bila ya mafanikio hivyo kurudi nyuma kimaendeleo.
Pia mbunge huyo alimuomba Waziri Mkuu kuwaondolea zuio la kuuza mazao yao nje ya nchi kwa sababu kitendo hicho kimesababisha kushuka bei ya mahindi na kusababisha hasara kubwa kwa wakulima ambao wametumia gharama kubwa katika kuandaa mashamba.
Akizungumzia zuio hilo Waziri Mkuu alisema lengo la Serikali kuzuia uuzwaji wa mazao nje ni kutaka kujiridhisha na uwepo wa chakula cha  kutosha nchini ili kuepuka kukumbwa na baa la njaa na kisha kwenda kuomba msaada kwenye nchi tuliowauzia.
Kuhusu suala la soko la mahindi Waziri Mkuu alisema Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) watanunua kwa bei ya soko na kwamba wataruhusiwa kuuza nje ya nchi baada ya Serikali kujaza maghala yake huku wataalam wakimalizia kufanya tathmini ya hali ya chakula nchini.
Habarika zaidi na P5TANZANIA.BLOGSPOT.COM

Comments

Popular posts from this blog

HISTORIA FUPI YA ABDULRAHMAN KINANA ALIYEJUZULU UKATIBU MKUU CCM

FAHAMU HISTORIA YA JOKETI ALIYETUMBULIWA NA UVCCM

HISTORIA FUPI YA LAZARO NYALANDU ALIYEIBWAGA CCM NA KUHAMIA CHADEMA