WAKURUGENZI WATAKIWA KUWAHAMASISHA WALIMU KUJIENDELEZA KIELIMU
Na.Issack Gerald Bathromeo-Rukwa
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Wakurugenzi wa
halmashauri na Maofisa Elimu nchini kutowaondoa katika nyadhifa zao Waratibu wa
Elimu Kata na Wakuu wa shule za sekondari wasiokuwa na shahada, walimu wakuu wa
shule za msingi wasiokuwa na diploma badala yake wawahamasishe kwenda kusoma.
Agosti 20 mwaka huu Waziri Mkuu alisema Waratibu
wa Elimu katika ngazi ya Kata na Wakuu wa shule za sekondari wanatakiwa kuwa na
shahada huku walimu wakuu kwenye shule wanatakiwa kuwa na diploma.
Waziri
Mkuu ametoa agizo hilo jana jioni wakati akizungumza na wananchi katika mkutano
wa hadhara uliofanyika kwenye kiwanja cha Mandela katika jimbo la Sumbawanga
mjini.
Alisema Mratibu wa Elimu katika ngazi ya Kata ni
lazima awe na shahada ili aweze kutekeleza majukumu yake ya kusimamia utolewaji
wa elimu katika shule za sekondari na msingi.
Alisema katika kuboresha maslahi ya walimu Serikali
imetenga zaidi ya sh. bilioni tano kwa mwezi ambazo ni posho ya madaraka. Waratibu
Elimu Kata wanapewa sh 250,000 kwa mwezi huku Wakuu wa shule za sekondari na
walimu wakuu katika shule za msingi wanapewa sh. 200,000.
Waziri Mkuu alisema badala ya kuwaondoa kwenye
nyadhifa hizo ni vema Wakurugenzi wakawahamasisha walimu hao kwenda kusoma ili
na wao wanufaike na posho ya madaraka iliyoanza kutolewa na Serikali hivi
karibuni.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu
amewataka wazazi na walezi kwenda kuwaandisha watoto wenye umri wa miaka mitano
katika shule za awali ambapo watapata fursa ya kujengewa msingi mzuri wa masomo
kabla ya kuanza darasa la kwanza.
Pia aliagiza shule zote za msingi nchini zisizokuwa na
madarasa ya awali kuhakikisha waanzisha madarasa hayo haraka na kuanza kutoa
elimu hiyo.
Habarika zaidi na P5TANZANIA.BLOGSPOT.COM
Comments