AFARIKI DUNIA BAADA YA KUFUKIWA NA KIFUSI AKICHIMBA DHAHABU NSIMBO KATAVI
Na.Issack Gerald-Mpanda
Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina Mateo
Robert(33) mchimbaji mdogo mkazi wa Mbeya-Songwe,amefariki dunia baada ya
kuangukiwa na lundo la udongo akiwa kwenye shimo (LONG BASE) wakati akichimba
madini ya dhahabu.
Kamanda
wa polisi Mkoani Katavi Dhahiri Kidavashari amesema kuwa tukio hilo limetokea Mnamo
tarehe 23.12.2015 majira ya saa 09:00 kwenye Machimbo ya dhahabu ya wachimbaji
wadogo ya Nsimbo yaliyopo kijiji cha Katuma, Kata ya Katuma, Tarafa ya Mwese Wilaya
ya Mpanda Mkoa wa Katavi.
Kamanda amesema kuwa marehemu akiwa na
wenzake wawili ambao ni Edson David Akiba(25 mchimbaji Mkazi wa Kigoma pamoja
na Tungu Thomas(30) mchimbaji Mkazi wa mkoa wa Shinyanga walielekea mgodini
hapo kufanya shughuli zao za uchimbaji kama ilivyo kawaida yao ambapo wakati wa
uchimbaji huo marehemu na mwenzake aitwaye Tungu Thomas walikuwa wameingia
shimoni na nje shimo walimuacha mwenzao ambaye ni Edson David Akiba ambapo
baada ya muda mfupi kilisikika kishindo kutoka ndani ya shimo.
Kutokana na hali hiyo Edson David alijaribu kuwaita wenzake
waliokuwa shimoni hawakuitika ndipo harakati za kuwasaidia zilipofanyika kwa
kuwaita wachimbaji wengine wa maeneo jirani ambapo baada ya kuingia marehemu
alikutwa kafunikwa na udongo akiwa tayari kafariki dunia huku mwenzake Tungu
Thomas akiwa amejeruhiwa kichwani.
Aidha Kamanda Kidavashari amesema,kwa mujibu
wa uchunguzi wa kitabibu kifo cha marehemu kilitokana na majeraha aliyoyapata
kichwani (HEAD INJURY) na mwili wake ulikabidhiwa kwa ndugu zake kuendelea na
taratibu zingine za mazishi, huku Tungu Thomas akipatiwa matibabu katika hospitali ya Katuma
na kuruhusiwa kwenda kujiuguzia nyumbani.
Hata hivyo si mara ya kwanza matukio kama
haya kutokea ikizingatiwa kuwa hivi karibuni wachimbaji wadogo walifukiwa
katika mgodi wa Nyangalata uliopo Wilayani Kahama.
Comments