WANANCHI WALALAMIKIA UONEVU KATAVI
Wananchi wa kitongoji cha Itogolo
katika kijiji cha Kampuni kata ya
misunkumilo Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda Mkoani Katavi,wameilalamikia
serikali kuwakamata,kuwatoza faini na kuwalazimisha kuvuna mazao yao kabla ya
kukomaa.
Wananchi hao wakiwemo Agnes John,Charles
Pius na Peter Luamula wametoa malalamiko hayo katika mkutano wa hadhara wa
kijiji cha Kampuni ambapo ulikuwa ukifanyika katika kitongoji hicho lengo
likiwa ni kutoa nafasi kwa wananachi kueleza kero zao.
Wamesema wamekuwa wakikamatwa ovyo na
mgambo kisha kupelekwa mahabusu na kulipishwa faini wakati hakuna elimu ya
kutambua mita sitini kutoka chanzo cha maji ya mto Mpanda iliyotolewa.
Kwa upande wao wajumbe wa kamati ya
watumia maji bonde la mto Mpanda Mahela Mahanda na Daudi Sumuni wamekanusha
kuwaamrisha wananchi kuvuna mazao yao kabla ya kukomaa lakini wamekubali
kuwakamata na kuwatoza faini kabla ya kutoa elimu kwa wananchi hao.
Mwenyekiti wa kijiji cha Kampuni
Bw.James Simoni amesema mpaka sasa watu watatu wamekamatwa na kutozwa faini
katika kitongoji hicho chenye kaya zipatazo 71 zinazotegemea mto Mpanda kuendesha
maisha yao.
Hata hivyo naye amekiri kuwa elimu
katika kitongoji hicho ilikuwa haijatolewa lakini amesema wananchi hao walikuwa
na taarifa tangu mwaka jana.
Comments