TANZANIA YATAKIWA KUUNGA MKONO MGOGORO WA URUSI NA UINGEREZA
Serikali ya Uingereza imeitaka
Tanzania na Jumuiya ya Kimataifa kuiunga mkono katika kupinga kitendo cha Urusi
kutumia sumu aina ya novichok katika jaribio la kumuua jasusi wa Kirusi Sergei
Skripal na binti yake Yulia.
Akizungumza na vyombo vya habari
jijini Dar es Salaam jana, Balozi wa Uingereza hapa nchini Sarah Cooke alisema
nchi yake haitavumilia majaribio yoyote ya mauaji ya watu wasio na hatia ndani
ya ardhi yake.
Cooke alisisitiza kuwa ni wazi Urusi
ilihusika katika jaribio hilo na walipewa nafasi ya kueleza kwa nini waliamua
kutumia sumu hiyo ndani ya Uingereza licha ya kwamba matumizi ya kemikali kama
silaha ni kinyume cha sheria za kimataifa. Hata hivyo,alisema mpaka sasa hawajatoa
maelezo kuhusu suala hilo.
Alipoulizwa kuhusu msimamo wa
Tanzania kuhusu suala hilo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje,Dk Susan Kolimba
alisema hawezi kulizungumzia kwa sasa ambapo hata Waziri wa Mambo ya Nje,Dk
Augustine Mahiga hakupatikana ili kuzungumzia suala hilo .
Mpaka sasa Uingereza inaungwa mkono
na Marekani, Ufaransa,Ujerumani,Austalia na Umoja wa Kujihami wa Nchi za
Magharibi (Nato) ambapo pia imeripoti suala hilo katika Baraza la Usalama la
Umoja wa Mataifa.
Kufuatia hatua hiyo,Waziri Mkuu wa
Uingereza,Theresa May ametangaza kwamba hakuna waziri yeyote au mtu kutoka
familia ya kifalme atakayehudhuria Fainali za Kombe la Dunia zinazotarajiwa
kufanyika Juni huko Urusi.
Tukio hilo la matumizi ya kemikali za
sumu lilitokea mwishoni mwa wiki iliyopita huko Salisbury Uingereza na kwa sasa
Skripal na Yulia wana hali mbaya hospitali.
Hata hivyo Uingereza tayari
imewatimua maofisa 23 wa intelijensia wa Urusi na imefuta ziara ya Waziri wa
Mambo ya Nje wa Urusi Sergey Lavrov.
Habari zaidi ni P5TANZANIA.BLOGSPOT.COM
Comments