MAHAKAMA YA RUFAA YAWAKANA CHADEMA
Mahakama ya Rufaa imesema hakuna
rufaa ya uchaguzi wa Jimbo la Longido iliyopo mahakamani hapo.
Mahakama hiyo imetoa kauli hiyo
wakati Chadema ikiilalamikia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuhusu kufanyika
uchaguzi mdogo wa ubunge wa jimbo hilo kwa madai kwamba kuna kesi mahakamani
hapo.
Uchaguzi huo mdogo ulifanyika baada
ya aliyekuwa mbunge wa Longido kwa tiketi ya Chadema Onesmo ole Nangole ushindi
wake kutenguliwa na Mahakama Kuu.
Mara kadhaa Mwenyekiti wa Chadema,Freeman
Mbowe na Ole Nangole wamekaririwa na vyombo vya habari wakidai kuna rufaa
katika Mahakama ya Rufani.
Viongozi hao wamekuwa wakiilalamikia
NEC kuwa iliendesha uchaguzi mdogo katika jimbo hilo wakati rufaa ya kupinga
hukumu ya Mahakama Kuu iliyomvua ubunge Ole Nangole ikiwa haijatolewa uamuzi.
Hata hivyo,Mahakama ya Rufaa imesema
uchaguzi mdogo uliofanyika Longido ulikuwa halali kwa kuwa hakuna rufaa yoyote
iliyoko mahakamani hapo.
Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufaa,Elizabeth
Mkwizu amesema hakuna rufaa yoyote ya kupinga hukumu ya uchaguzi wa Longido
iliyoko mahakamani hapo bali kuna maombi.
Kwa mujibu wa ratiba ya vikao vya
Mahakama ya Rufaa, maombi hayo yamepangwa kusikilizwa na Jaji Jacob Mwambegele
Februari 5 mwaka huu.
Wakati wa usikilizwaji wa maombi
hayo,mwombaji kupitia kwa mawakili wake atalazimika kutoa sababu za kuiridhisha
Mahakama ni kwa nini alichelewa kuwasilisha taarifa ya kusudio la kukata rufaa.
Ikiwa Mahakama haitaridhika na sababu
zake itatupilia mbali maombi hayo lakini ikiridhika nazo itamruhusu kuwasilisha
taarifa ya kusudio la kukata rufaa.
Baada ya kuwasilisha taarifa hiyo,atasubiri
kupata kumbukumbu za rufaa,yaani nyaraka zitakazohusika kwenye rufaa yake ikiwamo
hukumu anayoilalamikia,mwenendo wa kesi ya msingi na vielelezo vilivyotumika.
Akipata nyaraka hizo,ndipo
atakapowasilisha rufaa kamili,yaani sababu za kwa nini anapinga hukumu iliyomvua
ubunge wa jimbo hilo na upande wa pili (wajibu rufaa) nao utawasilisha hoja
zake na baada ya Mahakama kusikiliza hoja za pande zote ndipo itatoa hukumu.
Ole Nangole alivuliwa ubunge na
Mahakama Kuu Kanda ya Arusha Juni 29,2016 kutokana na kesi ya uchaguzi
iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea wa kiti hicho kwa tiketi ya CCM,Dk Steven
Kiruswa akipinga ushindi wake.
Baada ya Mahakama kumvua ubunge,Ole
Nangole kupitia mawakili John Materu na Dancan Oola aliwasilisha taarifa ya
kusudio la kukata rufaa kupinga hukumu hiyo.
Hata hivyo,taarifa hiyo ya kusudio la
kukata rufaa ilitupiliwa mbali na Mahakama kutokana na kasoro za kisheria.
Baada ya kutupiliwa mbali,kwa kuwa
muda wa kisheria wa siku 14 za kuwasilisha kusudio la kukata rufaa ulikuwa
umeshaisha, waliwasilisha maombi ya kuongezewa muda wa kuwasilisha taarifa
hiyo.
Maombi hayo pia yalitupiliwa mbali na
Mahakama Kuu Kanda ya Arusha,ndipo wakapeleka maombi Mahakama ya Rufani.
Habari zaidi ni P5TANZANIA LIMITED
Comments