DK.SLAA AKUTANA NA RAIS IKULU JIJINI DAR,MAAFISA WASTAAFU WA JWTZ NAO WAAGANA NA RAIS

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. John Pombe Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi Mteule Mhe.Dkt. Wilbrod Peter Slaa Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Baada ya Mazungumzo hayo Balozi Mteule Mhe.Dkt. Slaa amemshukuru Mhe.Rais Magufuli kwa kumuamini na kumteua kuwa Balozi na ameahidi kuwa yupo tayari kutekeleza majukumu atakayopangiwa kwa kutanguliza maslahi ya Taifa.
Mhe.Dkt.Slaa amempongeza Mhe.Rais Magufuli na Serikali yake ya Awamu ya Tano kwa uongozi bora wenye maono na uthubutu wa kutekeleza mambo makubwa yenye maslahi kwa nchi ikiwemo miradi mikubwa kama vile ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge),ujenzi wa daraja la juu (Flyover) katika makutano ya barabara ya Nyerere na Mandela (Tazara),mradi wa uzalishaji umeme katika maporomoko ya mto Rufiji (Stieglers’ Gorge) na mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi.
Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mhe. Dkt. Slaa kwa moyo wake wa kizalendo na amesema aliamua kumteua kuwa Balozi kwa kuwa anatambua kuwa ataweza kupigania maslahi ya Tanzania popote atakapopangiwa kuiwakilisha.
Wakati huo huo,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli ameagana na maafisa wakuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambao wanastaafu baada ya kutimiza umri.
Walioagana na Mhe.Rais Magufuli ni Luteni Jenerali James Mwakibolwa aliyekuwa Mnadhimu Mkuu wa JWTZ na Meja Jenerali Michael Isamuhyo aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Wengine ni Brigedia Jenerali Aron Lukyaa,Brigedia Jenerali William Kivuyo,Brigedia Jenerali Elizaphani Marembo na Kanali Peter Samegi.
Akizungumza baada ya kuagana,Luteni Jenerali Mwakibolwa amemshukuru Mhe.Rais Magufuli kwa kumteua kuwa Mnadhimu Mkuu wa JWTZ na amesema anaondoka na kuliacha jeshi likiwa na nidhamu,utii, uzalendo na weledi.
Kwa upande wake Meja Jenerali Isamuhyo pamoja na kumshukuru Mhe.Rais Magufuli  amesema anafurahi kuiacha JKT ikiwa imeimarika katika majukumu yake yakiwemo ujenzi wa viwanda,kilimo na kuimarisha mafunzo kwa vijana wazalendo.

 Habari zaidi ni P5TANZANIA LIMITED

Comments

Popular posts from this blog

HISTORIA FUPI YA ABDULRAHMAN KINANA ALIYEJUZULU UKATIBU MKUU CCM

FAHAMU HISTORIA YA JOKETI ALIYETUMBULIWA NA UVCCM

HISTORIA FUPI YA LAZARO NYALANDU ALIYEIBWAGA CCM NA KUHAMIA CHADEMA