DC MKOANI RUKWA APIGA MARUFUKU WAGONJWA WA KIPINDU PINDU KUPELEKWA KWA WAGANGA WA JADI
Mkuu wa wilaya ya Sumbawanga mkoani
Rukwa Dk.Halfan Haule amewataka wakazi wa bonde ziwa Rukwa,kuacha tabia ya
kuwapeleka wagonjwa wa kipindupindu kwa waganga wa kienyeji badala yake
wawapeleke vituo vinavyotoa huduma za afya ili kupata tiba za kitaalamu.
Mkuu huyo wa wilaya alisema hayo wakati
akizungumza na wananchi wa kata ya Mtowisa wilayani Sumbawanga mkoani humo.
Alisema tabia ya baadhi ya wananchi
kuendekeza imani za kushirikina na kuwapeleka wagonjwa wa kipindupindu kwa
waganga wa kienyeji kunahatarisha maisha ya wagonjwa hao na wakati mwingine
kusababisha vifo.
Alisema jamii ya watu wa bonde la
ziwa Rukwa ambako ugonjwa huo umeenea ipo haja sasa kubadilika na kuachana na
tabia hiyo kwani ugonjwa huo unatokana na uchafu na si kulogwa hivyo wanapaswa kuwapeleka wagonjwa katika zahanati,vituo vya afya na hospitali
ili wapate tiba sahihi ambazo zitaokoa maisha yao.
Aidha Dk.Haule alipiga marufuku tabia
ya kaya moja kutumia choo kimoja badala yake alitaka kila kaya kuwa na choo
chake na kaya isiyokuwa na choo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi
yake.
Awali,mganga mkuu wa wilaya hiyo,Fani
Mussa alisema tangu ugonjwa wa kipindupindu uripotiwe katika halmashauri hiyo
siku 53 zilizopita,jumla ya wagonjwa 165 wameugua na kulazwa katika vituo
vinavyotoa huduma ya afya ambapo nane
kati yao wamefariki dunia.
Alisema hatua mbalimbali
zimechukuliwa ikiwa pamoja na kuchukuliwa kwa sampuli 15 ambazo zilithibitisha
kuwa na ugonjwa huo hivyo kusambaza dawa na vifaa tiba katika kambi mbalimbali
zilizofunguliwa kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa hao.
Alisema elimu ya afya inayolenga
kuwahamasisha wananchi kuzingatia kanuni za afya,ikiwa pamoja na kuchemsha maji
kabla kunywa na kunawa mikono baada kutoka chooni imetolewa kwa wakazi wa bonde
la ziwa Rukwa ambalo vijiji vyake vingi vimeathirika na malazi hayo.
Dk.Mussa alisema watu 14 kati ya 58
Waliokamatwa kwa kukiuka kanuni za afya ikiwa pamoja na kaya zao kutokuwa na
vyoo wamehukumiwa kifungo cha miezi mitatu jela.
Habari zaidi ni P5TANZANIA LIMITED
Comments