POLISI,JAJI MKUU WATOA ONYO MGOMO WA MAWAKILI HAPA NCHINI-Agosti 28,2017
Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma na Jeshi
la Polisi nchini,wamelionya Baraza la Uongozi la Chama cha Mawakili wa
Tanganyika (TLS),kutoingilia vyombo vya uchunguzi na upelelezi,vinavyochunguza
tukio la mlipuko,uliotokea kwenye ofisi za Kampuni ya Mawakili ya IMMMA usiku
wa kuamkia juzi jijini Dar es Salaam.
Profesa Juma jana alisema TLS hawana haki ya kutoa agizo
kwa mawakili, kutohudhuria mahakamani na kwenye mabaraza mengine, kwa kuwa kila
wakili ana mkataba binafsi na mteja wake.
Profesa Juma alisema uhuru wa mahakama ni pamoja na kuheshimu
mamlaka nyingine za nchi zinapokuwa zinafanya kazi zake.
Alisema kwa kuwa tukio la kulipuliwa kwa ofisi za Mawakili wa
Immma ni tukio la kihalifu, hivyo wanasheria waiache Polisi na vyombo vingine
vya upelelezi kufanya kazi yao.
“Kama kutatokea wateja watakaolalamika kuwa mawakili wao
hawakufika mahakamani siku ya Jumanne na Jumatano, hatua za kisheria dhidi ya
mawakili hao zitachukuliwa ikiwemo kuwapeleka kwenye Kamati ya Maadili ya Mawakili,” alieleza Kaimu
Jaji Mkuu.
Kwa upande wao,Jeshi la Polisi limesema liachwe liendelee na
kazi ya uchunguzi, badala ya kulihusisha na tukio hilo.
Msemaji wa Jeshi hilo Makao Makuu, Kamishina Msaidizi Barnabas
Mwakalukwa alisema Jeshi la Polisi ndicho chombo chenye mamlaka ya kufanya
uchunguzi na hivyo kama kuna mtu yeyote mwenye taarifa yoyote kuhusu tukio
hilo, anatakiwa kuzitoa polisi badala ya kuzungumza na vyombo vya habari.
Kauli hizo za Polisi na ya Kaimu Jaji Mkuu, zimekuja baada ya
Rais wa TLS, Tundu Lissu kuwaeleza waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuwa
Baraza lao la Uongozi lina taarifa kuwa kikundi cha watu wenye silaha za moto,
wakiwa wamevalia sare za Jeshi la Polisi, kiliwateka nyara walinzi binafsi wa
Kampuni ya IMMMA na kuingia ndani ya eneo la ofisi hizo.
Lissu alidai watu hao baada ya kuingia ndani, walitega milipuko
na madumu manne ya mafuta ya petroli katika maeneo kadhaa ya jengo la ofisi
hizo.
Alidai muda mfupi baadaye, milipuko hiyo ililipuka na
kusababisha uharibifu mkubwa wa jengo la ofisi za IMMMA Advocates zilizoko
Upanga pamoja na majengo jirani.
“Kama Lissu ana hizo taarifa alitakiwa azilete polisi kwa kuwa
ndicho chombo cha uchunguzi badala ya kuzungumza na vyombo vya habari.
"Kazi ya polisi ni kufanya uchunguzi wa kina na ndiyo maana
Kaimu Kamanda wa Kanda Maalumu alisema atatoa taarifa uchunguzi ukikamilika,
hivyo watu wanapaswa kusubiri taarifa kamili, nje ya hapo tunakuwa tunafanya
kazi nje ya utawala wa sheria,” alieleza Msemaji wa Jeshi la Polisi, Mwakalukwa.
Mwakalukwa alivitaka vyombo vya habari, kuwatafuta walinzi hao
ambao Lissu alidai walitekwa na watu wanaodhaniwa kuwa polisi ili waeleze tukio
lilivyokuwa na ikibidi walinzi hao kutoa taarifa za kutekwa kwao polisi.
Alisema jambo hilo siyo dogo, hivyo watu waviache vyombo vya
uchunguzi, viendelee na kazi yake kwani uchunguzi pekee ndiyo utakaobaini
chanzo na wahusika.
Ili kuonesha mshikamano, Baraza la Uongozi la TLS limewataka
mawakili wote ambao ni wanachama wao nchini, wasuse kuhudhuria mahakamani na
kwenye mabaraza ya aina zote kwa siku mbili, kesho na keshokutwa.
Comments