ONA HUU UTUMBUAJI MAJIPU RUKWA,KESHO WAPI?ENDELEA KUFUATILIA P5 TANZANIA MEDIA


Sumbawanga
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe amewasimamisha kazi maofisa watano wa Idara ya Misitu mkoani Rukwa kwa kushindwa kusimamia vema na kudhibiti uvunaji haramu wa magogo.       
Baadhi ya magogo yaliyopelekea utumbuaji majipu kufanyika(PICHA NA.Issack Gerald)
                                                               

Waliosimamishwa ni Kaimu Meneja wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), Nyanda za Juu Kusini, Bruno Mallya na Mshauri wa Maliasili Sekretarieti ya Mkoa wa Rukwa, Nicholas Mchome kupisha uchunguzi.
Wengine waliosimamishwa kazi ni Ofisa Misitu wa TFS, Helman Ndanzi na Ofisa Misitu daraja la II, Geofrey Mwasomola wote kutoka wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa. Mwingine ni Meneja wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) Sumbawanga na Kalambo, Martin Hamis.
Profesa Maghembe alisema amelazimika kuwasimamisha kazi maofisa hao kwa kushindwa kusimamia vema na kudhibiti uvunaji haramu wa magogo aina ya mkurungu na kusababisha uharibifu mkubwa katika Msitu wa Kalambo.
Pia wanadaiwa kuruhusu makundi makubwa ya mifugo kuchungwa katika msitu huo bila kuchukua hatua stahiki kwa wavamizi. Aliwaagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa TFS, kuhakikisha maagizo hayo yanatekelezwa.
Profesa Maghembe alifanya ziara jana mkoani Rukwa na kufanya kikao cha ndani na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa mkoa mjini Sumbawanga kwa zaidi ya saa mbili. Baada ya kikao hicho, Profesa Maghembe alishuhudia shehena ya magogo ya mkurungu, yaliyokamatwa na kuhifadhiwa nje ya jengo la ofisi za Mkuu wa Mkoa.
Kisha alikwenda mjini Matai ambako ni Makao Makuu ya Wilaya ya Kalambo, alikoshuhudia shehena nyingine ya magogo ya mti huo wa mkurungu yamehifadhiwa katika Kituo cha Polisi wilaya ya Kalambo tangu Desemba mwaka jana.
Pia alishuhudia lori lenye namba za usajili T427 ASG lenye kontena lililokamatwa katika kituo cha forodha Kasesya kilicho katika mpaka wa Tanzania na Zambia, likisafirisha magogo hayo kwa vibali bandia likiwa limezuiliwa katika Kituo cha Polisi wilayani Kalambo.
Vile vile alikwenda hadi katika Misitu wa Kalambo unaomilikiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo ambako alishuhudia uharibifu mkubwa uliosababishwa na uvunaji haramu wa magogo.
Magogo ya mkurungu yenye thamani zaidi ya Sh milioni 100, yalikuwa yamevunwa kinyume cha sheria.
Waziri aliwapatia TFS wiki moja kuhakikisha magogo yaliyovunwa katika msitu wa Kalambo, yenye thamani ya Sh bilioni 500, yanasafirishwa na kuhifadhiwa katika kituo cha polisi.
Magogo hayo sasa yamehifadhiwa katika vijiji vinne vya Kasitu, Safu Jengeni na Kaluko vinavyozunguka Msitu wa Kalambo.

Comments

Popular posts from this blog

HISTORIA FUPI YA ABDULRAHMAN KINANA ALIYEJUZULU UKATIBU MKUU CCM

FAHAMU HISTORIA YA JOKETI ALIYETUMBULIWA NA UVCCM

HISTORIA FUPI YA LAZARO NYALANDU ALIYEIBWAGA CCM NA KUHAMIA CHADEMA