SERIKALI YAWASIMAMISHA KAZI WATENDAJI WAKALA WA VIPIMO TANZANIA
Na.Issack Gerald
SERIKALI
imeamua kuwasimamisha kazi watendaji wawili kutoka Wakala wa Vipimo nchini (WMA)
kuanzia leo ili kupisha uchunguzi wa upotevu wa mafuta bandarini kutokana na
zuio la kufunga kwa mita kwa zaidi ya miaka mitano.
Waziri mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa akipata maelezo bandarini jana Februari 11 kutoka kwa watendaji katika bandari hiyo |
Waliosimamishwa
kazi ni Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo nchini (WMA), Bi. Magdalena Chuwa na
Meneja Vipimo Kitengo cha Bandari, Bi. Bernadina Mwijarubi. Bi. Mwijarubi ndiye
anashughulikia kitengo cha mafuta bandarini.
Akitangaza
uamuzi huo kwenye kikao cha Makatibu Wakuu kilichofanyika leo Februari 12,
2016) ofisini kwake Magogoni jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk. Adelhelm Meru
awaandikie barua za kuwasimamisha kazi ili kupisha uchunguzi huo.
“Katibu
Mkuu Viwanda, waandikie barua za kuwasimamisha kazi ili kupisha uchunguzi.
Katika kipindi hiki hawatatakiwa kusafiri kwenda popote hadi uchunguzi
utakapokamilika. Pia utafute mtu wa kukaimu nafasi hiyo ili kazi ziendelee,”
alisema.
Waziri
Mkuu pia amesema ofisi yake itawaandikia barua ofisi ya TAKUKURU na polisi ili
wafuatilie suala hilo mara moja na ikithibitika kuwa walihusika hatua rasmi
zitachukuliwa na itathibitika hawakuhusika basi watarudishwa.
Waziri
Mkuu pia aliagiza mfumo wa upimaji mafuta kwa kutumia flow meters
uendelee kutumika na ule upimaji wa kukadiria uache kutumiwa mara moja.
Jana
(Alhamisi, Februari 11, 2016) Waziri Mkuu alifanya ziara kukagua flow meters
za zamani zilizopo Kurasini (Kurasini Oil Jetty) na kisha akatembelea na
kukagua flow meters mpya ambazo zinajengwa Kigamboni. Mita hizo
zimegharimu dola za marekani milioni 6 (sawa na sh. bilioni 12.96/- za sasa).
Pia
Waziri Mkuu alitembelea sehemu ya kuchukulia mafuta yanayotoka bandarini (TPA
Manfold) iliyoko Kigamboni na kukagua mitambo ya kusambazia mafuta kwenye
matenki ya mafuta ya kampuni ya TIPER yaliyoko Kigamboni yanayomilikiwa kwa
ubia baina ya Serikali na kampuni ya Oryx Energies.
Katika
ziara hiyo ilibainika kuwa Kampuni ya TIPER imejiunganishia bomba la moja kwa
moja kutoka kwenye bomba kubwa la mafuta linalotoka bandarini hali iliyomlazimu
Waziri Mkuu kuagiza kwamba bomba hilo litolewe kwenye maungio hayo ndani ya
mwezi mmoja.
“Jana
niliagiza kuwa bomba hilo ling’olewe. Nimetoa mwezi mmoja ili kurekebisha mfumo
huo. Simamieni vizuri na kuhakikisha kuwa na wao pia wanarudi kwenye manfold
kama ilivyo kwa wengine,” alisema Waziri Mkuu.
Comments