KESI YA KUVUNJA DUKA YAENDELEA KULINDIMA MPANDA,HAKIMU ATUPILIA MBALI OMBI LA MSHTAKIWA
Na.Issack Gerald-Mpanda
KESI ya kuvunja
duka na kuiba nguo zenye thamani ya shilingi milioni moja na laki nne na elfu
arobaini, inayomkabili Bw. Reuben Remmy mkazi wa Makanyagio,mwishoni mwa wiki
ya Januari,imeendelea kusikilizwa katika mahakama ya Mwanzo mjini Mpanda.
Ushahidi
uliotolewa mbele ya Hakimu wa mahakama hiyo Bw. David Mbembela ni pamoja na
vielelezo vya makufuli mawili yaliyovunjwa siku ya tukio usiku wa tarehe 28
mwezi desemba mwaka jana mjini Mpanda.
Shahidi wa sita
askari wa jeshi la polisi Mpanda kitengo cha upelelezi, Selcius Mosha,
ameithibitishia mahakama kuwa vielelezo hivyo ni sahihi na vimetambuliwa na
mlalamikaji Bi. Rosana Mwancheta pamoja na mashahidi wengine.
Hakimu Mbembela
amesema mahakama imetupilia mbali pingamizi lililotolewa na mshtakiwa la
kuiomba isitambue vielelezo hivyo, na kwamba mshtakiwa ana kesi ya kujibu.
Kesi hiyo
imeahirishwa hadi tarehe 15 mwezi Februari mwaka huu itakaposikilizwa tena.
Comments