WAZIRI MKUU AWASILISHA TAARIFA YA MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA KAZI ZA SERIKALI
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema mpa akufikia Februari 2018 Serikali ya Awamu ya
Tano imeanzisha viwanda vipya 3,306.
Ametoa
kauli hiyo leo Bungeni mjini Dodoma,wakati akiwasilisha taarifa ya mapitio ya
utekelezaji wa kazi za Serikali kwa mwaka 2017/2018 na mwelekeo wa kazi za
Serikali kwa mwaka 2018/2019 kwenye mkutano wa 11 wa Bunge.
Amesema
Serikali inahamasisha uwekezaji katika viwanda kwa kutoa vivutio vya kodi na
visivyo vya kodi kwa wawekezaji mahiri wa kuendeleza na kuboresha miundombimu
wezeshi kama vile barabara,reli,bandari, umeme na maji.
Aidha
Waziri Mkuu amelieleza Bunge kuwa mikoa na Halmashauri zote nchini zimeelekezwa
kutenga maeneo ya uwekezaji kwa ajili ya viwanda na kwamba katika mwaka
2018/2019,Serikali itatoa kipaumbele katika kutekeleza miradi ya kielelezo,uanzishwaji
wa kanda maalum za kiuchumi pamoja na kuboresha mazingira ya biashara na
kuvutia uwekezaji katika sekta ya viwanda.
Akitoa
ufafanuzi kuhusu ushiriki wa sekta ya hifadhi ya jamii kwenye ujenzi wa uchumi
wa viwanda,Waziri Mkuu amesema pamoja na miradi mingine NSSF na PPF kwa
kushirikiana na Jeshi la Magereza wanatekeleza mradi mkubwa wa uzalishaji wa
sukari mkoani Morogoro.
Waziri
Mkuu alisema tangu kuanza kwa utekelezaji wa mradi huo Juni 2017,ajira za moja
kwa moja 780 na ajira zisizo za moja kwa moja 24,000 ikijumuisha wakulima
wadogo wa mbegu na kilimo cha nje zimezalishwa.
Akifafanua
kuhusu ujenzi wa barabara kuu,Waziri Mkuu alisema Serikali inaendelea kuboresha
mtandao wa barabara nchini ambapo katika kipindi cha Julai 2017 hadi Februari
2018,ujenzi wa Km.776.45 za barabara kuu kwa kiwango cha lami umekamilika na Km.
1,760 zinaendelea kujengwa huku barabara zenye urefu wa Km.17,054 zikikarabatiwa
katika kipindi hicho.
Kuhusu
ujenzi wa madaraja,Waziri Mkuu alisema madaraja ya Kilombero na Kavuu ujenzi
wake umekamilika na kwamba ujenzi unaoendelea hivi sasa ni wa madaraja ya
Sibiti,Mto Mara,Lukuledi,Ruhuhu,Momba na Mlalakuwa ambapo madaraja mengine 996
katika maeneo mbalimbali nchini yamekarabatiwa.
Kuhusu
jitihada za Serikali kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dar es
Salaam,Waziri Mkuu alisema hadi kufikia Februari 2018,ujenzi wa barabara ya juu
katika eneo la TAZARA ulikuwa umefikia asilimia 70 na ujenzi wa barabara za juu
katika makutano ya Ubungo umeanza.
Katika
hatua nyingine,Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuliarifu Bunge juu ya
uanzishwaji wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tanzania Rural and
Urban Roads Agency – TARURA) kwa lengo la kurahisisha huduma za usafirishaji na
kuongeza kasi ya wananchi kujiletea maendeleo.
Waziri
Mkuu aliliomba Bunge likubali kupitisha shilingi. 143,618,762,698 zikiwa ni
makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi
zilizopo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2018/2019 ambapo shilingi
74,527,321,698 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. 69,091,441,000 ni kwa
ajili ya matumizi ya maendeleo.
Vilevile,Waziri
Mkuu aliliomba Bunge liidhinishe shilingi 125,521,100,000 kwa ajili ya Mfuko wa
Bunge ambapo shilingi 117,205,487,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi
8,315,613,000 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
Habari zaidi ni www.p5tanzania.blogspot.com
Comments