RAIS MAGUFULI ASISITIZA SERIKALI KUSHIRIKIANA NA VIONGOZI WA DINI KULETA MAENDELEO
Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli amesema Serikali
ya Awamu ya Tano itaendelea kushirikiana na viongozi wa dini katika masuala
mbalimbali ya maendeleo hapa nchini.
Rais
Magufuli ametoa kauli hiyo leo katika Ibada ya kumsimika Mhashamu
Askofu Isaac Amani kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha iliyofanyika
katika viwanja vya Kanisa la MtakatifuTeresia wa Mtoto Yesu Jijini Arusha.
Mhashamu Askofu Isaac
Amani aliyekuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Moshi aliteuliwa na Baba Mtakatifu
Francis tarehe 27 Desemba,2017 kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo hilo na amesimikwa na
Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha Mhashamu Josephat Louis
Lebulu na Balozi wa Baba Mtakatifu hapa nchini Askofu Mkuu Marek Solczynski.
Hatua ya rais Rais
Magufuli kuhudhuria ibada hii ya kanisa katoliki imechukuliwa kama ishara bora
ya kurejesha uhusiano mwema na baadhi ya makanisa makuu ya kikristo likiwemo
kanisa katoliki ambao wamekua wakiikosoa vikali serikali yake.
Katika
hatua nyingine,Mh.Rais Magufuli amechangia mifuko 300 ya saruji kwa ajili ya
ujenzi Kanisa Kuu jipya la Mtakatifu Teresia wa Mtoto Yesu ambalo ujenzi wake
unaendelea.
Katika risala iliyosomwa
na Padre Alois Kitomari kwa niaba ya familia ya Mungu Jimbo Kuu Katoliki la
Arusha, imempongeza rais Magufuli kwa juhudi zake za kusimamia vizuri nidhamu
ya utumishi wa umma na utendaji wa taasisi za umma,kukabiliana na ufisadi,
uzembe na ubadhilifu wa mali za umma,vita dhidi ya rushwa,ujenzi wa
viwanda,bandari,madini na uboreshaji wa sekta ya usafiri kwa kujenga reli ya
kisasa,ununuzi wa ndege na ujenzi wa barabara.
Hata hivyo kwa upande
wake Mhashamu Askofu Isaac Amani ambaye amesimikwa amesema,ni vigumu kutenganisha
siasa na dini.
Ibada ya kusimikwa kwa Askofu Mkuu Isaac Amani imehudhuriwa na
Maaskofu 33 wa Kanisa Katoliki,Mke wa Rais Mhe.Mama Janeth Magufuli,Waziri Mkuu
Mstaafu Mhe.Mizengo Pinda,Spika Mstaafu Mhe.Anne Makinda,viongozi wakuu wa
vyombo vya ulinzi na usalama,Wabunge,Viongozi wa Mkoa wa Arusha wakiongozwa na
Mkuu wa Mkoa Bw.Mrisho Gambo na wananchi wa Arusha.
Habari zaidi ni www.p5tanzania.blogspot.com
Comments