KWA MWAKA 2017 WAPO WENGI WALIOTUMBULIWA NA RAIS MAGUFULI,HAWA NI BAADHI YA VIGOGO
Katika
mwaka 2017, mambo mengi yametokea ambayo yametikisa nchi kuanzia kwenye nyanja
ya kijamii, kiuchumi, kisiasa na hata kiutamaduni. Imekuwepo mijadala mikubwa
sana kuanzia kwenye ajali za barabarani, uchumi wa nchi, utawala, na mambo
mengine yanayogusa maisha ya wananchi.
Rais Dkt John Magufuli |
Wakati
zikiwa zimesalia siku 6 mwaka 2017 kuisha, na mjadala sasa ukiwa ni sikukuu za
Christmas na Mwaka Mpya na suala la Wachagga kurudi makwao, tutakuwa
hatujautendea haki kama, japo kwa ufupi hatutakumbushana masuala yaliyotokea kwenye
siasa kwa mwaka huu.
Mwaka
huu, neno “Kutumbua” lilishika kasi sana. Hii ni kutokana na Rais Magufuli
ambaye alisema amejipa kazi ya kutumbua majipu, kuwafuta kazi viongozi ambao
kwake yeye aliona hawaendani na kasi yake au kutokana na sababu nyingine
yoyote. Idadi ya waliotumbuliwa ni wengi, na katika mjadala wetu wa leo,
tutaangazia vigogo 12 waliotumbuliwa tangu Januari 1, 2017.
1. Mhandisi
Felchesmi Mramba.
Januari
Mosi 2017, Rais Dk. John Magufuli, alitengua uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji
wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Felchesmi Mramba. Hatua
hiyo ilikuja siku moja baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na
Maji (EWURA), kutangaza kuridhia ombi la TANESCO la kupandisha bei ya umeme kwa
asilimia 8.5 kutoka 18 waliyoomba.
Kutokana
na kutenguliwa kwa Mramba, Rais Dk. Magufuli alimteua Dk. Tito Mwinuka kutoka
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kuwa Kaimu Mkurugenzi wa TANESCO.
2. Nape
Moses Nnauye
Machi
23 mwaka huu, Rais Dkt John Pombe Magufuli alifanya mabadiliko ya baraza la
mawaziri ambapo aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo, Nape
Moses Nnauye aling’olewa na nafasi yake kuchukuliwa na Dkt. Harrison Mwakyembe.
Kutumbuliwa
kwa Nape kulikuja siku moja baada ya kupokea ripoti kutoka kwa kamati aliyokuwa
ameiunda kwa ajili ya kuchunguza sakata la kuvamiwa kwa Ofisi za Clouds
Media Group.
3. Prof. Sospeter Muhongo
Miezi
7 iliyopita (24 Mei, 2017), Rais Dkt. John Pombe Magufuli alitengua
uteuzi wa Waziri wa Nishati na Madini (sasa Wizara ya Nishati na Wizara ya
Madini), Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo. Licha ya kuwa barua kutoka Ikulu
haikueleza sababu ya utenguzi wake, lakini wakati akipokea ripoti ya makinikia,
Rais Magufuli alimtaka Waziri Muhongo ajiuzulu kwa kushindwa kusimamia suala la
mchanga wa dhahabu unaosafirishwa kwenye makontena.
Lakini
Waziri Muhongo nae aliandika barua kwenda kwa Rais Magufuli akieleza kwamba
amejiuzulu nafasi yake ya uwaziri kufuatia mapendekezo yaliyotolewa na kamati
iliyofanya uchunguzi wa makinikia.
4. George
Simbachawene
Septemba
7, aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa, George Simbachawene aliandika barua ya kujiuzulu wadhifa huo baada
ya kutajwa katika ripoti za uchunguzi wa biashara ya madini ya Tanzanite
na Almasi iliyoonyesha namna serikali lilivyopoteza matrilioni ya fedha
kutokana na sababu mbalimbali.
Kujiuzulu
kwake kulikuja muda mfupi tangu Rais Magufuli kuwataka viongozi wote aliowateua
na wametajwa katika ripoti hiyo wakae pembeni ili kupisha uchunguzi ambao
utakuwa huru na wa haki.
5. Mhandisi Edwin Amandus Ngonyani
Kama
ilivyokuwa kwa Simbachawene aliyejiuzulu baada ya kutakiwa kupisha uchunguzi,
aliyekuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin
Ngonyani naye alijiuzulu Septemba 7 baada ya kutuhumiwa kutotekeleza majukumu
yake kikamilifu alipokuwa akifanya kazi katika Shirika la Madini la Taifa
(STAMICO) lenye dhamana ya kusimamia madini.
6. Prof.
Justin Ntalikwa
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Joseph Pombe Magufuli alitengua
uteuzi wa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Prof. Justin Ntalikwa
kuanzia tarehe 26 Machi 2017.
Profesa
Ntalikwa alifutwa kazi na Rais Magufuli siku chache baada ya kufanya ziara ya
kushtukiza bandarini.
Mei
2017, Rais Magufuli alisema kwamba, alimfuta kazi kiongozi huyo kutokana na
kueleza Kamati ya Bunge kiasi ambacho kilikuwa kipo kwenye makontena ya dhahabu
ambacho hakikuwa sawa.
7. Prof. Jumanne Abdallah Maghembe
07
Oktoba, 2017 alifanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri kwa kuongeza idadi
ya Wizara, kuteua Mawaziri na Naibu Mawaziri wapya na kuwahamisha Wizara baadhi
ya Mawaziri na Naibu Mawaziri.
Aliyekuwa
Waziri wa Mali Asili na Utalii, Prof. Maghembe aliachwa nje ya uteuzi au
mabadiliko hayo ambapo nafasi yake ilichukuliwa na aliyekuwa Naibu Waziri wa
Wizara ya Afya, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamisi Andrea Kigwangalla.
8. Mhandisi
Ramol Makani
Katika
mabadiliko ya baraza la mawaziri yaliyofanywa na Rais Dkt Magufu Oktoba 7,
2017, Mhandisi Makani aliachwa nje na nafasi yake kuchukuliwa na Josephat
Ngailonga Hasunga.
Mhandisi
Ramol Makani alikuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii. Hakuna
maelezo yoyote yaliyotolewa kuhusu kutumbuliwa kwa Makani.
9. Anastasia
Wambura
Wambura
alikuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo.
Kiongozi huyo aliachwa nje ya mabadiliko ya baraza la mawaziri na nafasi yake
ikachukuliwa na Juliana Daniel Shonza.
10. Dkt.
Charles Mlingwa
Mlingwa
alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara ambapo Oktoba 26 mwaka huu Rais Magufuli
alifanya mabadiliko na kumuondoa, kisha nafasi yake kuchukuliwa na Adam
Kigoma Malima.
11. Jordan
Rugimbana
Katika
mabadiliko ya Oktoba 26, Rais Dkt Magufuli alimuacha nje, aliyekuwa Mkuu wa
Mkoa wa Dodoma, Joardan Rugimbana na kumteua Bi Christine Solomon
Mndeme kuchukua nafasi hiyo.
Licha
ya kuwa Mndeme alipangiwa Mkoa wa Dodoma, Rais Magufuli alimtaka akaanzie kazi
Mkoa wa Shinyanga, na hivyo aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab
Tellack akahamishiwa Dodoma.
Kabla
ya uteuzi huo, Bi. Mndeme alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini.
12. Halima
Dendego
Dendego
alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara. Katika mabadiliko yaliyofanyika, nafasi
yake ilichukuliwa na Gelasius Gasper Byakanwa.
Kabla
ya uteuzi huo, Byakanwa alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai.
Mbali
na ambao uteuzi wao ulitenguliwa au kuachwa nje ya mabadiliko yaliyofanyika,
wengine wengi walitumbuliwa lakini Rais alitangaza kuwa watapangiwa kazi
nyingine. Baadhi ya wanaoangukia katika kundi hili ni Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba Erasto Mfugale na Mkurugenzi wa Halmashauri
ya Wilaya ya Bukoba Vijijini Mwantum Dau.
Rais
alitengua uteuzi wa wakurugenzi hao baada ya kushindwa kujibu maswali yake
mbele ya wananchi.
Habari zaidi ni P5TANZANIA LIMITED
Comments