KASI YA KUMNASUA MTOTO WA KIKE HASA MIMBA ZA UTOTONI YAZIDI KUSHIKA KASI
Na.Issack Gerald
WATOTO wa kike mkoani Rukwa
wamepewa mafunzo maalumu ya namna ya kuzitambua changamoto mbalimbali
zinazowakwamisha kuzitumia fursa zilizopo katika kutekeleza matarajio yao ili
waweze kujitegemea.
Akizungumza katika uzinduzi wa
mradi uitwao U-report unaotekelezwa na Tanzania Girl Guides Association
mkufunzi wa mradi huo,Emiliana Stanslaus amesema wahitimu wapatao 20 katika
kila halmashauri wamewezeshwa namna ya kuwasaidia wasichana wenzao katika
kukabiliana na vitendo vya ukatili dhidi yao.
Amesema wasichana hao walipata
mafunzo ya siku mbili ambapo watawasaidia wanafunzi wenzao wa kike katika shule
za msingi na sekondari na wasichana waliopo vijijini katika kukabiliana na
changamoto mbalimbali katika maisha yao ikiwa ni pamoja na kubakwa na pia
kupata mimba za utotoni.
Emiliana amesema mradi huo
utatekelezwa katika halmashauri za Sumbawanga vijijini,Kalambo,Nkasi na
Sumbawanga Manispaa kwa njia ya kutuma ujumbe wa maandishi ya simu kwenda namba
maalumu ya 15070 kwa mitandao yote na kunawawezesha walengwa kutoa taarifa
kwenye vyombo na mamlaka zinazohusika dhidi ya vitendo vya ukatili
walivyofanyiwa wasichana hao.
Tanzania Girl Guides Association
kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na watoto
ulimwenguni UNICEF-inatarajia kutoa mafunzo kwa wasichana zaidi ya 15 elfu
watakaosaidia kuwaelimisha wenzao katika mikoa ya hapa nchini namna ya
kukabiliana na vitendo vya ukatili.
Kwa upande wake Honorotha Wamai ambaye
ni mkufunzi wa Girl Guides mkoani Rukwa amesema wasichana hao waliohitimu
wanatakiwa kutoa mafunzo yanayohusu mradi huo katika halmasahuri zao za wilaya
kwa kushirikiana na idara za elimu na maendeleo ya jamiii.
Awali akizindua mradi huo kwa
niaba ya katibu tawala mkoa wa Rukwa,mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya
wilaya ya Sumbawanga John Msemakweli amesema serikali imetunga sheria
zinazowalinda wasichana dhidi ya vitendo vya ukatili.
Amesema katika utekelezaji wa
sheria hizo,serikali mkoani Rukwa itawafikisha mahakamani wazazi ambao watoto
wao wanapata ujauzito pindi itakapobainika kuwa wameshiriki kuficha ukweli au
vielelezo vitakavyosaidia kuwatia hatiani watuhumiwa wa kuwapa mimba
mwanafunzi.
Habari zaidi na P5TANZANIA LIMITED
Comments