ASILIMIA 90 YA WACHIMBAJI MADINI MKOANI KATAVI WANACHIMBA MADINI BILA UTAFITI
Na.Issack Gerald-Katavi
Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya
Magharibi Mhandisi Juma Haruna Sementa,amesema asilimia 90 ya wachimbaji wa
madini Mkoani Katavi,wanashindwa kufikia malengo katika uchimbaji madini kutokana
na sababu mbalimbali ikiwemo kutofanya utafiti kabla ya kuchimba.
Mhandisi Sementa amesema hayo wakati akizungumzia kuhusu baadhi maeneo ya uchimbaji kutelekezwa
ikiwemo maeneo ya Kapalamsenga.
Ametaja sababu nyingine inayokwamisha
uchimbaji endelevu wa madini mkoani Katavi kuwa ni ukosefu wa mtaji wa fedha za
kuendeshea mitambo.
Katika hatua nyingine Kamishna
Sementa amesema ujenzi wa kituo cha mfano cha kuchenjua madini kilichokuwa
kimepangwa kukamilika ujenzi wake mwezi Septemba mwaka huu katika machimbo ya
Kapanda,bado haujatekelezwa kutokana na uhaba wa fedha.
Hata hivyo ametaja shughuli za
uchimbaji madini bila utafiti ndiyo chanzo kinachopelekea uharibifu wa
mazingira.
Baadhi ya maeneo yanayotajwa kuwa na
madini hususani dhahabu Mkoani Katavi ni pamoja na Kapanda,Katisunga, Kapalamsenga, Machimboni, Katuma
na Isulamilomo na Kasekese.
Comments