ZIARA YA WAZIRI MKUU WILAYANI TANGANYIKA : WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA AAGIZA KUONDOLEWA WATU WALIOVAMIA MAENEO YALIYOHIFADHIWA
Na.Issack Gerald Bathromeo-Tanganyika
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameuagiza uongozi wa wilaya
ya Tanganyika mkoani Katavi kuhakikisha unawaondoa watu wote wanaoishi katika
maeneo ya hifadhi na ushoroba wa wanyama wa Lyamgoroka.
WAZIRI Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa |
Agizo hilo limetolewa jana jioni na Waziri Mkuu wakati
akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kiwanja
cha Majalila wilayani Tanganyika.
Waziri Mkuu alisema wilaya hiyo inatakiwa kuendelea kuwaondoa watu
wote waliovamia na kujenga makazi ndani ya Hifadhi ya Taifa ya
Katavi ili kuepuka uharibifu wa mazingira.
“Hakikisheni mnatunza mazingira. Msiache wakate miti hovyo kwa
sababu wanakausha vyanzo vya maji na kusababisha eneo kuwa hatarini kukumbwa na
ukame, hivyo ni vyema wakaondolewa mapema,” alisema.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amewataka Maofisa Ushirika na Kilimo katika mkoa wa
Katavi kuwasaidia wakulima wa tumbaku kwa kuhakikisha wanapata soko la uhakika
na kulipwa kwa wakati.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo baada ya kupokea malalamiko ya
wananchi kupitia mabango waliyokuwa wameyabeba ambayo yalikuwa yakiwalalamikia
maofisa hao kwa kushindwa kuwatafutia masoko na badala yake
wanawakumbatia wabadhilifu wa fedha za ushirika.
"Hatuwezi kuwa na Ofisa Kilimo ambaye hajui masoko ya mazao
ya wakulima wake.Mnakaa ofisini tu! Hamfanyi kazi. Lazima mfuatilie masuala ya
kilimo katika maeneo yenu, sasa chukua mabango yote yanayohusu zao la tumbaku
na ukalete majibu kwa wakulima,” alisema.
Awali Waziri Mkuu alitembelea eneo lililotengwa kwa ajili ya
ujenzi wa ofisi za halmashauri na wilaya Tanganyika ambapo aliwapongeza wakazi
wa kijiji cha Majalila kwa kutoa bure ardhi yenye ukubwa wa ekari 500 ili
Serikali iweze kujenga ofisi hizo.
Habarika zaidi na P5TANZANIA.BLOGSPOT.COM
Comments