ZIARA YA WAZIRI MKUU WILAYANI MLELE :FANYENI UKAGUZI KUBAINI WALIOKULA FEDHA ZA USHIRIKA NA KUWACHUKULIA HATUA
Na.Issack Gerald Bathromeo-Inyonga Mlele
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemtaka Mkuu wa Mkoa Katavi,
Meja Jenerali (Mstaafu) Raphael Muhuga kupeleka wakaguzi wilayani Mlele na
kubaini watu waliokula fedha za chama cha ushirika cha Ukonongo na kuwachukulia
hatua.
Waziri Mkuu akiwa ziarani Inyonga wilayani Mlele baada ya kutawazwa kuwa Chifu wa Wakonongo(PICHA NA.Issack Gerald) |
“Watakaobainika watiwe hatiani. Licha ya bodi ya ushirika
huo kuvunjwa, hatuwezi kuacha suala hili limalizike kwa kuvunja bodi kwa sababu
walioingia wanaweza kuiba kwa mategemeo ya kuvunjwa bodi,“ amesema.
Waziri
Mkuu ametoa agizo hilo jana wakati akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa
hadhara uliofanyika katika kiwanja cha Inyonga wilayani Mlele.
Amesema kila mtumishi afanye kazi na awajibike kwa
uadilifu na uaminifu mkubwa kwa mujibu wa taaluma yake ili kuhakikisha wananchi
wanapata maendeleo kwani hilo ndilo lengo la kuajiriwa kwake.
“Haiwezekani hapa kuna Ofisa Ushirika halafu Waziri Mkuu
analetewa mabango ya kumtaka atatue tatizo la chama cha Ushirika. Hali hii
inaonyesha hapa hakuna kazi inayofanyika,“ amesema.
Waziri Mkuu amesema wanahitaji watumishi watakaosikiliza
maelekezo yanayotolewa na Serikali na kuyafanyia kazi kwa sababu malengo ya
Mhe. Rais Dk. John Magufuli ni kuona nchi hii inabadilika hivyo wasioweza ni
vema wakaandika barua za kuacha kazi.
“Msikubali kuhamasishwa kufanya mambo yatakayowaletea
madhara. Fanyeni kazi ili tupate maendeleo. Hatuwezi kufananishwa na nchi ndogo
ndogo, wenzenu wanafanya kazi nasi tupunguze maneno tufanye kazi,“ amesema.
Wakati huo huo Waziri Mkuu amesema Serikali
imedhamilia kumaliza changamoto ya upatikanaji wa umeme nchini ambapo imetenga
zaidi ya sh. trilioni moja kwa ajili ya kumalizia kazi ya usambazaji umeme nchi
nzima ikiwemo wilaya ya Mlele.
Amesema watapeleka jenereta kubwa mbili zitakazofungwa
katika kijiji cha Utende ambazo zitasambaza na kuwasha umeme katika kata ya
Inyonga na maeneo mengine.
“Mwezi Novemba mwaka huu umeme utakuwa umewaka wilayani
Mlele. Mkakati ni kuunganisha mkoa wa Katavi na gridi ya Taifa kutoka Tabora,
kupita Sikonge hadi Inyonga,“ amesema.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji na
mbunge wa jimbo la Katavi, Mhandisi Isack Kamwelwe amemuomba Waziri Mkuu
kuwasaidia kupandishwa hadhi kwa kituo cha afya cha Inyonga na kuwa Hospitali
ya wilaya kwa sababu wilaya yao haina hospitali.
Pia ameomba wilaya hiyo ipatiwe umeme wa Tanesco ili kupunguza
gharama kubwa za kununua umeme kutoka kwa mfanyabiashara ambaye amefunga
jenereta na anawauzia unit moja sh. 1000 wakati Tanesco wanauza sh. 100 kwa
unit moja.
Awali Mkuu wa wilaya ya Mlele, Rachel Kassanda alisema
wilaya hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya ukosefu wa nyumba
za watumishi hali inayosababisha mkuu wa wilaya na Katibu tawala wa wilaya
kuishi kwenye nyumba za kupanga.
Habarika zaidi
na P5TANZANIA.BLOGSPOT.COM
Comments