WAZIRI MKUU AAGIZA HATUA ZICHULIWE KWA WATUMISHI NCHINI WANAOIBA DAWA
Na.Issack Gerald Bathromeo-Katavi
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewataka wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri
nchini kuwachukulia hatua watumishi wote wa sekta ya afya wanaojihusisha na
wizi wa dawa.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitembelea hospitali ya wilaya ya Mpanda akiwa katika siku ya kwanza ya ziara ya mkoa wa Katavi Agosti 21, 2016. (Picha na Issack Gerald)Agosti 20,2016 |
“Fuatilieni
na kuwachukulia hatua watumishi wa Zahanati wanaoiba dawa. Hawa hawana nafasi
ya kuendelea kufanya kazi kwa sababu ni wauaji,” alisema.
Waziri
Mkuu ametoa agizo hilo jana jioni wakati akipokea taarifa ya mkoa wa Katavi
mara baada ya kuwasili mkoani hapa kwa ziara ya kikazi ya siku tatu.
Alisema
kila kiongozi kwenye eneo lake ahakikishe dawa zinazopelekwa na Serikali kwa
ajili ya kuwahudumia wananchi zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Pia ameitaka Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kujenga duka la
dawa mkoani Katavi kwa ajili ya kurahisisha upatikanaji wa dawa katika mkoa huu
pamoja na mikoa jirani.
Wakati huo huo Waziri Mkuu
aliwataka Waratibu wa Elimu katika ngazi ya Kata na Wakuu wa shule za sekondari
wasiokuwa na shahada waende wakasome kama wanahitaji kuendelea kuwa na wadhifa
huo.
Alisema Mratibu wa Elimu katika ngazi ya Kata ni
lazima awe na shahada ili aweze kutekeleza majukumu yake ya kusimamia utolewaji
wa elimu katika shule za sekondari na msingi.
Kwa upande wa walimu wakuu katika shule za msingi,
Waziri Mkuu alisema ni lazima wawe na diploma, hivyo aliwataka walimu wakuu
wote wasiokuwa na diploma kwenda kusoma kabla hawajaondolewa kwenye wadhifa
huo.
Alisema Serikali imetenga zaidi ya sh. bilioni tano
kwa mwezi ambazo ni posho ya madaraka, ambapo Waratibu Elimu Kata wanapewa sh
250,000 kwa mwezi huku Wakuu wa shule za sekondari na walimu wakuu katika shule
za msingi wanapewa sh. 200,000.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Katavi Meja Jenerali
(Mstaafu) Raphael Muhuga alisema mkoa umeendelea kuongeza bajeti ya dawa
ili kuhakikisha dawa zinapatikana katika ngazi zote za kutolea huduma.
“Mwaka 2012 bajeti ya dawa na vifaa tiba ilikuwa sh.
Milioni 558 ambayo ilitosheleza upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa asilimia
70. Katika bajeti ya mwaka 2016/2017 mkoa umetengewa jumla ya sh bilioni 1.3
ambayo tunaamini itamaliza tatizo la upatikanaji wa dawa na vifaa tiba,”
alisema.
Mkuu huyo wa mkoa alisema mfumo mpya wa usambazaji
dawa kupitia MSD umesaidia dawa, vifaa tiba na vitendanishi kupelekwa moja kwa moja
hadi katika ngazi ya zahanati hali iliyosaidia dawa kufika kwenye vituo
vya kutolea huduma kwa asilimia 100.
Mapema leo Waziri Mkuu amefanya ziara katika hospitali
ya Manispaa ya Mpanda ambapo amesema Serikali itahakikisha hospitali hiyo
inaongezewa huduma zaidi kwa sababu ni ya wilaya ila inahudumia wagonjwa wa
mkoa wote.
Habarika zaidi na P5TANZANIA.BLOGSPOT.COM
Comments