HABARI WIKI HII KUTOKA IKULU YA RAIS
1.AGIZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe
Magufuli amewaagiza viongozi wa Jeshi la Polisi Tanzania kuwaondoa watumishi
wote wasiokuwa askari polisi na ambao wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya
ukiukwaji wa taratibu na ufujaji wa fedha za umma ili kulinda heshima, nidhamu
na uadilifu ndani ya jeshi hilo.
Rais Magufuli ametoa maelekezo hayo leo tarehe 18 Julai, 2016
muda mfupi baada ya Naibu Makamishna wa Polisi 25 na Makamishna Wasaidizi
Waandamizi wa Polisi 35 kula kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma, Ikulu
Jijini Dar es salaam.
Pamoja na kutoa agizo la kutaka wasio askari polisi
kuondolewa katika utumishi wa jeshi la polisi, Rais Magufuli pia ameagiza jeshi
hilo lichukue hatua dhidi ya wote wanaokabiliwa na tuhuma za wizi wa fedha
wakiwemo wanaodaiwa kuiba mabilioni ya shilingi zilizotolewa kwa ajili ya
ununuzi wa sare za askari mwaka jana 2015.
"Mnajua kupeleleza, mna vyombo vyote, ofisi ya
IGP (Inspekta
Jenerali wa Polisi) ipo palepale, ofisi ya DCI (Mkurugenzi wa
Upelelezi wa Makosa ya Jinai) ipo palepale, Makamishna wote mnazunguka
mnakwenda palepale, mwizi mnae palepale, mnashindwa kumshika.
"Kama mnafikiri kuwa na raia katika jeshi la
polisi wanawaharibia kazi zenu hamisheni raia wote na wapelekeni utumishi,
kwani hakuna mhasibu ambaye ni askari polisi? hakuna mhandisi ambaye ni askari
polisi? hakuna afisa tawala ambaye ni askari polisi? Mimi nafikiri kama
matatizo ya wizi na wafanyakazi hewa yanaletwa na raia waliomo ndani ya jeshi
la polisi na majeshi yetu mengine, IGP kaorodheshe raia wote wanafanya kazi
Jeshi la Polisi ili waondolewe na tuwapangie kazi nyingine uraiani" Amesema Rais Magufuli
Hata hivyo Rais Magufuli amelipongeza Jeshi la Polisi kwa
kazi nzuri linayofanya iliyoliwezesha kujenga imani kubwa kwa watanzania na
ametaka viongozi wa Jeshi hilo wawaongoze askari walio chini yao vizuri, wawatie
moyo na waache vitendo vya kuwakatisha tamaa kwa kuwaadhibu ama kuwatisha pale
wanapochukua hatua stahiki dhidi watu wanaovunja sheria.
"Sasa mimi niwaombe nyinyi, wale wadogo
mnaowaongoza mkawape mamlaka ya kutimiza wajibu wao, hata kama ameshika gari la
IGP liache lishikwe IGP atakwenda kujieleza mwenyewe, hata akishika gari la RPC
afanye hivyohivyo, hata akishika gari la Waziri au gari la Rais mwacheni
atekeleze wajibu wake, sheria ni msumeno, tunawanyima nguvu hawa wa chini
wanapotimiza wajibu wao kwa mujibu wa sheria halafu unamwambia liachie,
ukifanya hivyo aliyeshikwa anatoka pale akiwa anatamba kwelikweli na yule
askari unamvunja nguvu ya kufanya kazi" Amesisitiza Rais Magufuli.
Rais Magufuli pia amelitaka jeshi hilo kuungana na vyombo
vingine vya serikali katika kutekeleza shughuli zake zikiwemo kusimamia
ukusanyaji wa mapato ya serikali bandarini, katika sekta ya utalii na maeneo
mengine, kukabiliana na vitendo vya rushwa na kuondoa watumishi hewa.
Tukio hili la Naibu Makamishna wa Polisi na Makamishna
Wasaidizi Waandamizi wa Polisi kula kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma
limeongozwa na Kamishna wa Maadili Jaji Mstaafu Salome Kaganda na limehudhuriwa
na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Mwigulu
Lameck Nchemba, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora Mhe.
Anjellah Kairuki, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Hamad Yusuf
Masauni, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. George Mcheche Masaju, Makatibu
Wakuu na Viongozi wa vyombo vya Ulinzi na Usalama.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
18 Julai, 2016
………………………..
2.UTEUZI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe
Magufuli amemteua Prof. Sylvester Michael Mpanduji kuwa Mkurugenzi Mkuu wa
Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO).
Taarifa iliyotolewa leo Ikulu Jijini Dar es salaam na Katibu
Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi imeeleza kuwa uteuzi wa Prof. Sylvester
Michael Mpanduji umeanzia leo tarehe 18 Julai, 2016.
Kabla ya uteuzi huu Prof. Sylvester Michael Mpanduji alikuwa
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA).
Prof. Sylvester Michael Mpanduji anachukua nafasi iliyoachwa
wazi na Mhandisi Omary Jumanne Bakari ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John
Pombe Magufuli amemteua Dkt.Winnie Mpanju-Shumbusho kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa
Hospitali ya Benjamini Mkapa - Dodoma.
Kabla ya Uteuzi huo, Dkt. Winnie Mpanju-Shumbusho alikuwa
Mkurugenzi Mkuu Msaidizi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) lenye makao yake
makuu Mjini Geneva nchini Uswisi na alimaliza mkataba wake tangu Mwezi Desemba
2015.
Uteuzi wa Dkt. Winnie Mpanju-Shumbusho umeanza leo tarehe 18
Julai, 2016.
Dkt. Winnie Mpanju-Shumbusho anachukua nafasi iliyoachwa wazi
na Dkt. Donan William Mmbando ambaye ameomba kupumzika kutokana na sababu
binafsi.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
18 Julai, 2016
………………………..
3.MIKOPO
Benki ya Exim ya China imekubali kutoa mkopo wenye masharti
nafuu wa dola za Marekani Bilioni 7.6 sawa na zaidi ya Shilingi Trilioni 16
za kitanzania kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa mradi mkubwa wa reli ya kati
hapa nchini kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) unaotarajiwa
kuanza katika mwaka huu wa fedha.
Rais wa Benki ya Exim ya China Bw. Liu Liang amemueleza Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 20
Julai, 2016 katika Ikulu ndogo ya Chamwino Mkoani Dodoma kuwa pamoja na kutoa
fedha hizo zitakazofanikisha ujenzi wa kilometa 2,190 za reli ya kati benki
hiyo itashirikiana na Tanzania katika kubadilishana uzoefu na utaalamu
katika ujenzi na uendeshaji wa reli.
Pamoja na kukubali kutoa fedha hizo, Rais huyo wa Benki ya
Exim ya China amempongeza Rais Magufuli na serikali yake kwa dhamira ya dhati
ya kuiletea nchi maendeleo ikiwemo kuharakisha ujenzi wa reli ya kati na
ameahidi kuwa benki yake itatoa ushirikiano wa karibu katika kufanikisha mradi
huo na miradi mingine ya maendeleo.
"Kuhusu huu mradi wa reli ya kati tuna mtazamo
chanya, tunauona ni mradi mzuri na tutatoa ushirikiano wowote utakaohitajika.
Tunaamini kuwa kwa ushirikiano na serikali ya Tanzania mchakato wa utekelezaji
wa mradi huu utafanyika kwa mafanikio na kwa kuzingatia muda" Amesema Rais Magufuli.
Kwa upande wake Rais Magufuli amemshukuru Rais wa Benki ya
Exim ya China Bw. Liu Liang kwa kukubali kutoa fedha hizo na amemuhakikishia
kuwa Tanzania imedhamiria kutekeleza mradi huo ambao tayari ujenzi wake
umepangwa kuanza katika mwaka huu wa fedha kwa kutumia fedha za ndani kiasi cha
shilingi Trilioni 1 zilizotengwa katika bajeti.
Rais Magufuli amebainisha kuwa kutekelezwa kwa mradi huo
kutasaidia kuinua uchumi wa Tanzania na nchi jirani zisizopakana na bahari
zikiwemo Uganda, Rwanda, Burundi, na Congo.
"Kwa hiyo kukubali kwao ambako ilikuwa ni kitu
kikubwa, inaonesha kwamba juhudi za Tanzania kwenda haraka haraka zinakubalika
kimataifa, na wenzetu hawa wachina wana pesa nyingi.
"Na kule kuaminika kwamba tunakopeshwa kwa
masharti nafuu, riba yake ni ndogo na huku kwetu ni mafanikio makubwa, kwa hiyo
mizigo mingi tutakuwa tunaisafirisha, tutaendeleza reli yetu na bandari
zetu" Amesema
Rais Magufuli.
Mradi wa ujenzi wa reli ya kati utahusisha ujenzi wa reli kwa
kiwango cha kisasa (Standard Gauge) kutoka Dar es
salaam-Tabora-Isaka-Mwanza, Tabora-Mpanda-Kalemela, Tabora-Uvinza-Kigoma
na Isaka-Keza-Msongati.
Mazungumzo kati ya Rais Magufuli na Rais wa benki ya Exim ya
China yamehudhuriwa na Balozi wa China hapa nchini Dkt. Lu Youqing, Waziri wa
Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa Mnyaa, Waziri wa Fedha na
Mipango Dkt. Philip Mpango na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki Dkt. Suzan Kolimba.
Gerson Msigwa
Kaimu
Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dodoma
20
Julai, 2016
Comments