WAZIRI MKUU APOKEA MISAADA YA MAAFA IRINGA YA SH. MILIONI 86/-
Na.Afisa habari
Ofisi ya Waziri Mkuu
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea misaada mbalimbali
yenye thamani ya sh. milioni 85.88/- kwa ajili ya wananchi walioathirika na
mafuriko kwenye vijiji vya kata ya Mlenge, tarafa ya Pawaga, wilaya ya
Iringa vijijini mkoa wa Iringa.
Misaada hiyo imetolewa na wadau mbalimbali kutokana na
mafuriko ambayo yalibomoa nyumba 82 katika kitongoji cha Kilala, kijiji cha
Kisanga na kuwaacha wananchi wake bila makazi.
Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kasanga ambako
alikwenda kukagua athari za mafuriko na kuwapa pole wananchi hao leo
mchana,Waziri Mkuu aliwashukuru wadau wote waliojitolea kuwachangia watu
waliopata maafa kutokana na mafuriko hayo.
Wadau waliotoa misaada hiyo ni Benki ya NMB mabati 500,
mifuko ya saruji 500, kilo 820 za maharage, kilo 750 za unga wa mahindi na lita
250 za mafuta ya kupikia vyote vikiwa na thamani ya sh. milioni 20/-. Wengine
ni Mfuko wa Pensheni wa PPF uliotoa mabati 200 na mifuko ya saruji 200
vyenye thamani ya sh. milioni 6.6/-.
Wengine ni Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF)
waliotoa mabati 200 na mifuko ya saruji 160 vyenye thamani ya sh. milioni
4.5/-; Kiwanda cha kusindika nyanya cha RedGold kimetoa mifuko ya saruji 100 na
mabati 50 vyenye thamani ya sh. Milioni 3/-; mbunge wa viti maalum kwa tiketi
ya CHADEMA, Bi. Susan Chogisasa na wenzake wametoa mabati 150, mifuko 23 ya
saruji, kilo 100 za maharage, kilo 50 za chumvi na nguo mbalimbali vyote
vikiwa na thamani ya sh. milioni 1.3/-.
Madiwani wa Iringa Vijijini walitoa sh. 380,000/-,
Wabunge wa Viti Maalum kupitia CCM walitoa vifaa vya sh. Milioni 1.7/-; ofisi
ya CCM Mkoa wametoa vifaa vya sh. milioni 6.1/-, Kamanda wa UVCCM Mkoa wa
Iringa, Bw. Salim Abri aliipatia Halmashauri ya Wilaya ya Iringa sh.
milioni 5/- ili wanunue vyakula vya waliopatwa na maafa.
Naye Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambaye pia ni mbunge wa Isimani, Bw. William Lukuvi alitoa fedha taslim sh. milioni 20/- kati ya hizo sh. milioni 15 zikiwa ni zake na milioni 5/- ni za Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Bw. George Simbachawene. Pia alikabidhi seti 251 za mashuka zenye thamani ya sh. milioni 4/- zikiwa ni mchango kutoka Benki ya CRDB.
Waziri Lukuvi ambaye alishatoa mabati 250, aliahidi kuongeza mabati mengine 250 (yote yana thamani ya sh. milioni 8), pia alikabidhi sh. milioni 1.5/- kwa diwani wa Mlenge ili ziwasaidie kukodi gari la kukarabati barabara yao ambayo imeharibika sana kutokana na mafuriko hayo.
Mapema, akitoa taarifa ya maafa kwa Waziri
Mkuu, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Bi. Amina Masenza alisema jumla ya kaya 82
zilikosa makazi kutokana na mvua zilizonyesha Februari 12 na kusababisha
mafuriko. Kabla ya hapo, kaya nyingine 75 zenye wakazi 377ziliathirika kutokana
na mvua zilizoanza Februari 3, mwaka huu.
Alisema miundombinu ya barabara na ya maji safi
iliharibiwa vibaya na kusababisha hasara ya zaidi ya sh, milioni 250/-. Pia
wakazi hao walikubwa na uginjwa wa kipindupindu kutokana na mto Mapogoro
kufurika na kusomba baadhi ya vyoo vya wakazi hao.
“Tangu Februari mosi, wamekkkwishapokea waginjwa wa
kipindupinda 351 llakini walioko wodini hivi sasa ni wagonjwa 25 tu,“ alisema
Mkuu huyo wa mkoa.
Comments