OFISA ELIMU AKANUSHA WANAFUNZI 21 KUTIMULIWA WAKITUHUMIWA KUVAA YEBOYEBO AMBAZO PIA ZILICHOMWA MOTO.
Na.Issack Gerald
WANAFUNZI
wapatao 21 wanaosoma Shule ya Msingi Kilambo cha Mkolechi, Kata ya Kala mwambao
mwa Ziwa Tanganyika wilayani Nkasi, wamefukuzwa shule kwa muda usiojulikana kwa
kuvaa viatu maarufu yeboyebo.
Imeelezwa
kwamba yeboyebo hizo zilikusanywa na kuchomwa kwa kile kilichoelezwa kwamba ni
kunatokana na waraka uliotolewa na Ofisa Elimu Halmashauri ya Nkasi (Msingi)
ukipiga marufuku wanafunzi kuvaa aina hiyo ya viatu shuleni.
Hata
hivyo,akizungumza kwa njia ya simu akiwa mjini Namanyere wilayani Nkasi mkoani
Rukwa, Ofisa Elimu Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi (Msingi), Misana Kwangula,
alikanusha kutoa waraka huo kwa shule hiyo.
“Sina
taarifa rasmi ila (Jumatatu) jioni alinipigia simu mkazi mmoja akinitaarifu
kwamba kuna mwalimu wa shule ya msingi Kilambo cha Mkolechi amechoma moto viatu
vya wanafunzi kwa madai kuwa ofisa elimu (msingi) ametoa waraka kwamba
wanafunzi hawatakiwi kuvaa yeboyebo shuleni…
“Hakuna
waraka wala marufuku yoyote iliyotolewa, isitoshe sio sahihi hata kidogo wala
sio kitu kizuri kuchoma vifaa walivyonavyo wanafunzi…. Sasa kama amewachomea
wanafunzi hao viatu hivyo vya yeboyebo basi awanunulie viatu vya ngozi,”
alisema Kwangula.
Mkasa
huo wa wanafunzi hao kufukuzwa shule na kuchomewa yeboyebo walizovaa ulitokea
juzi wakati wanafunzi hao walipofika shuleni wakiwa wamevaa viatu hivyo.
Inaelezwa kwamba mwalimu wa zamu, Baraka Mwakasege aliwazuia kuingia darasani,
badala yake akawaamuru wavue viatu vyao.
Taarifa
kutoka shuleni hapo zinaeleza kuwa, baada ya hatua hiyo, mwalimu huyo wa zamu
alizikusanya yeboyebo na kuzitia kiberiti kisha akawafukuza wanafunzi hao kwa
muda usiojulikana hadi wazazi na walezi watakapowanunulia viatu vya ngozi.
Mwalimu
Mkuu wa shule hiyo, Posian Ally alikanusha kumtuma mwalimu wa zamu kuwafukuza wanafunzi
hao shule kwa muda usiojulikana wala kuteketeza kwa moto yeboyebo zao. Alisema
ataitisha kikao ili kujadili suala hilo na kwamba mwalimu huyo akibainika
kutenda kosa hilo ataamriwa kuwanunulia watoto hao viatu vingine.
Akizungumza
mmoja wa wazazi wa wanafunzi hao, Privatus Yoram, alithibitisha kutokea kwa
mkasa huo. “Jana jioni nilimwona mwanangu anayesoma darasa la tano shuleni hapo
akirudi nyumbani akiwa peku.
Nikamuuliza
kulikoni, akanieleza kuwa mwalimu wa zamu (Mwakasege) amewafukuza shule na
kuchoma yeboyebo zao kutokana na waraka wa Ofisa Elimu Nkasi unaopiga marufuku
yeboyebo shuleni,” alisema Yoram.
Comments