IGP MANGU ATOA AGIZO KWA MAKAMANDA WA MIKOA YOTE NCHINI KUENDESHA OPARESHENI KALI DHIDI YA BODABODA
Na.Mwandihi
wetu-Dar es Salaam
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Ernest Mangu
amewataka Makamanda wa Polisi kote nchini kuendesha oparesheni kali ya
kuwachukulia hatua kali za kisheria waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda
wasiotii sheria za usalama barabarani ikiwemo kubeba abiria zaidi ya mmoja,
kupita katika taa nyekundu pamoja na kutovaa kofia ngumu.
IGP Ernest Mangu |
IGP Mangu alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na
Maafisa wakuu wa Polisi wakiwemo Makamanda wa Polisi wa mikoa, vikosi na makao
makuu katika kikao kazi kilichokuwa kikifanyika jijini Dar es Salaam ambacho
kilifunguliwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi.
Alisema waendesha bodaboda wamekuwa wakikaidi
kufuata sheria za usalama barabarani lakini sasa mwisho wao umefika na kuwataka
makamanda wa polisi wa mikoa kote nchini kutekeleza maelekezo hayo ili kuleta
nidhamu kwa bodaboda katika kufuata sheria za usalama barabarani.
IGP Mangu alisema suala la kufuata sheria za usalama
barabarani kwa bodaboda halina mjadala na kila kamanda ahakikishe kuwa wale
wote wasiofuata sheria na kukaidi wanakamatwa bila kuoneana muhali kwakuwa
wamekuwa wakisababisha ajali zinazoweza kuzuilika.
“ Pamoja na kuendelea kudhibiti uhalifu wa aina
zote, natoa maelekezo kwa kila mkoa kuhakikisha unaendesha
oparesheni kali dhidi ya bodaboda ili kupunguza ajali zinazosababishwa na
bodaboda ambao wengi wao hawataki kufuata sheria na kanuni za usalama
barabarani, tusiwaonee muhali maana maisha ya watu ni muhimu sana na jambo la
msingi ni kusimamia sheria tu” Alisema IGP Mangu.
Awali akifungua kikao kazi hicho Waziri wa Mambo ya
Ndani ya nchi Mh. Charles Kitwanga alilitaka Jeshi la Polisi kuendelea na
mapambano yake dhidi ya uhalifu na wahalifu ili usalama wa raia na mali zao
uendelee kuimarika na watanzania waendelee na shughuli zao za kujiletea maendeleo
bila hofu ya kutendewa uhalifu.
Pamoja na agizo hilo la IGP
Mangu,mwezi uliopita,Kamanda wa Polisi Mkoani Katavi Dhahiri Kidavashari
akizungumza na na alisema kuwa Oparesheni hili ilikwishaanza kuanzia mwanzoni
mwa mwezi Januari na mafanikio kadhaa yaliyojitokeza katika opaereheni hiyo ni
pamoja na kukamata silaha kadhaa kutoka kwa wanamiliki silaha kinyume na
sheria.
Comments