HOTUBA YA MHE. KASSIM MAJALIWA
MAJALIWA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA
KUHITIMISHA SHUGHULI ZA MKUTANO WA PILI WA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA
TANZANIA
TAREHE 5 FEBRUARI, 2016
|
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiahirisha mkutano wa pili wa bunge la Jamhuri ya muungano wa Tanzania bunge la 11 mjini Dodoma leo hadi Aprili 19 2016 utakapofanyika mkutano mwingine |
I:
UTANGULIZI
(a)
Masuala ya Jumla
Mheshimiwa
Naibu Spika,
1.
Kwanza nianze kwa kumshukuru Mungu
kwa kutujalia afya njema na uwezo katika kutenda yote yaliyo mema. Tumekuwepo
hapa kwa takriban siku 11 katika shughuli za Mkutano wa Pili wa Bunge lako
Tukufu. Ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu mwenye wingi wa Rehema kwa
kutufikisha salama siku ya leo.
2.
Tumekutana hapa tukiwa
tumeshuhudia uundwaji wa Serikali unaoendelea ambapo Mheshimiwa Dkt John
Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amefanya uteuzi wa
Baraza jipya la Mawaziri ambao ni Waheshimiwa Wabunge wenzetu. Niruhusu
nitumie nafasi hii ya awali kuwapongeza Mawaziri na Naibu Mawaziri wote ambao
wameteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali katika Serikali ya Awamu ya Tano.
(b)
Chaguzi Mbalimbali
Mheshimiwa
Naibu Spika,
3.
Katika Mkutano huu, tumeweza
kufanya Chaguzi za Wenyeviti na Makamu Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za
Bunge. Vilevile, tumefanya chaguzi za Wenyeviti wa Bunge letu na Wajumbe wa
kutuwakilisha katika Taasisi mbalimbali za Kitaifa na Kimataifa. Kwa vile
orodha ni ndefu, napenda nitumie nafasi hii kuwapongeza kwa dhati kabisa na
kwa ujumla wao wote waliogombea nafasi hizo na kushinda. Ni matarajio yangu
kwamba tutatumia nafasi hizo vizuri katika kuleta ushirikiano, mshikamano na
kufanya kazi pamoja kama Wawakilishi wa Wananchi na kutekeleza majukumu yetu
kama Wabunge ndani ya Bunge hili.
(c)
Maafa na Ajali
Mheshimiwa Naibu Spika,
4.
Tarehe 27 Januari, 2016 wakati
Bunge lako Tukufu likiendelea na Vikao, Waheshimiwa Wabunge walipewa taarifa
ya kusikitisha ya kuzama kwa Kivuko cha Kilombero, ambapo katika tukio hilo
watu walipoteza maisha na wengine kujeruhiwa. Aidha, mali za abiria
zimepotea. Wakati huo huo, mvua zinazoendelea kunyesha nchini katika baadhi
ya maeneo zimesababisha mafuriko, vifo, uharibifu wa mali ikiwemo mazao na
miundombinu. Katika baadhi ya maeneo, mvua hizi zimesababisha njaa na athari
nyingine kwa jamii.
5.
Pamoja na maafa ya mvua na
mafuriko, wapo wananchi waliofariki na wengine kupata ulemavu katika ajali
mbalimbali za vyombo vya usafiri. Nitumie fursa hii kuwapa pole wote
waliopoteza ndugu, jamaa na marafiki katika matukio yote hayo. Aidha, napenda
kuwatakia afya njema wote waliopata majeraha. Kwa wale wote waliopoteza
maisha tunawaombea Roho zao zilale mahali pema peponi - Amina.
6.
Kuhusu uharibifu wa miundombinu,
tunazo taarifa za uharibifu mkubwa wa Miundombinu katika maeneo kadhaa.
Napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba Serikali itafanya kila
liwezekanalo kurekebisha miundo mbinu ya barabara iliyoharibika. Tunatambua
gharama kubwa inayohitajika, lakini ni wajibu wetu kama Serikali kuhakikisha
Wananchi wanapata huduma muhimu hasa za mawasiliano kati ya eneo moja na
jingine.
(d)
Maswali
Mheshimiwa
Naibu Spika,
7.
Leo tunahitimisha Mkutano wetu wa
Pili wa Bunge tukiwa tumefanya shughuli mbalimbali ndani ya Bunge letu.
Katika Mkutano wetu, Waheshimiwa Wabunge wamepata fursa ya kuuliza maswali ya
kawaida na yale ya papo papo kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu. Jumla ya maswali 115
ya msingi na 307 ya nyongeza yaliulizwa
na Waheshimiwa Wabunge na kujibiwa na Serikali.
(e)
Mjadala wa Hotuba ya Rais
Mheshimiwa
Naibu Spika,
8.
Katika Mkutano huu moja ya agenda
iliyochukua nafasi kubwa ni Hoja ya Serikali ya kujadili Hotuba ya Mheshimiwa
Dkt. John Pombe Maufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hoja hiyo
tuliihitimisha vizuri na kwa mafanikio makubwa. Kazi kubwa iliyoko mbele yetu
ni kutekeleza yale tuliyokusudia kama wajibu wetu. Napenda kuwapongeza tena
Waheshimiwa Wabunge wote kwa kushiriki katika mjadala wa Hotuba hiyo vizuri.
Nichukue tena nafasi hii kuliahidi Bunge lako Tukufu kwamba michango ya
Waheshimiwa Wabunge na maoni yao yatazingatiwa kwa utekelezaji.
II: MPANGO WA TAIFA WA MAENDELEO
Mheshimiwa Naibu Spika,
9.
Katika Mkutano huu wa Bunge,
Waheshimiwa Wabunge wamepata fursa ya kujadili na kuidhinisha Mapendekezo ya
Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali katika mwaka wa Fedha
2016/2017. Vilevile, Bunge limejadili na kutoa maoni na ushauri katika
mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika mwaka wa Fedha,
2016/2017. Kipekee, naomba nimshukuru Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip
Isdor Mpango(Mb) na Naibu wake Dkt. Ashatu Kachwamba Kijaji (Mb.) pamoja na
Waheshimiwa Mawaziri wa Wizara za Kisekta kwa ufafanuzi mzuri walioutoa
wakati wa kuhitimisha hoja hii. Aidha, napenda kutumia fursa hii kuwapongeza
Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yao mizuri, maoni na ushauri ambao
Serikali itauzingatia katika kukamilisha maandalizi ya Mpango na Bajeti ya
mwaka 2016/2017.
Mheshimiwa Naibu Spika,
10.
Naomba nami uniruhusu nitoe
maelezo mafupi ya msisitizo katika maeneo machache yaliyopata michango mingi
kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge waliochangia hoja ya Serikali ya mapendekezo
ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo. Waheshimiwa Wabunge wengi wamesisitiza kuhusu
umuhimu wa Serikali kuongeza uwajibikaji katika ukusanyaji wa mapato ya
Serikali na kuimarisha udhibiti wa matumizi ya Serikali. Aidha, Waheshimiwa
Wabunge wameishauri pia Serikali kuweka kipaumbele cha ujenzi wa Reli mpya ya
Kati, kujenga uchumi wa Viwanda, kuanza na kusimamia ujenzi na Mitambo ya
kuchakata gesi asilia (LNG) na Kiwanda cha Mbolea Mkoani Lindi, kuongeza kasi
ya usambazaji wa umeme Vijijini, ujenzi wa Bandari Mtwara, kutatua changamoto
zinazowakabili Wakulima na Wafugaji pamoja na Wachimbaji Madini.
Vilevile, kuweka mikakati thabiti
ya utekelezaji wa Miradi ya Sekta za Elimu, Afya, Maji na huduma kwa wenye
Ulemavu na pia kuzingatia utawala bora. Serikali inatambua kuwa maeneo haya
ni muhimu sana katika kujenga uchumi imara na endelevu na pia kuondoa
umasikini. Hivyo, itazingatia sana ushauri huu mzuri uliotolewa na
Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Naibu Spika,
11.
Naomba nitumie fursa hii
kumpongoeza Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa umahiri mkubwa na
umakini aliouonesha ikiwa ni mwanzo mzuri wa kuongoza Serikali ya Awamu ya
Tano. Mheshimiwa Rais ameonesha kasi kubwa na dhamira ya dhati ya kuwatumikia
Watanzania katika kujenga uchumi imara, unaokuwa na endelevu. Waheshimiwa
Wabunge wengi watakubaliana nami kwamba Serikali ya Awamu ya Tano katika
kipindi chake cha mwanzo cha siku 100, imeonesha dhahiri nia ya dhati ya
kuhakikisha kwamba makusanyo ya mapato yetu yanaongezeka. Jitihada hizo za
kuongeza makusanyo ya mapato ya Serikali zimefafanuliwa vizuri kwenye Hotuba ya
Waziri wa Fedha na Mipango. Serikali itaendelea na mikakati yake ya kuongeza
Mapato yake na kudhibiti mianya ya kukwepa kodi. Ni matumaini yangu kuwa
Waheshimiwa Wabunge, Wafanyabiashara na Wananchi wote wataunga mkono dhamira
hiyo njema ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika,
12.
Kuhusu matumizi, tayari Serikali
imeanza kuchukua hatua thabiti za kudhibiti matumizi yasiyo na tija katika
Wizara, Idara za Serikali zinazojitegemea na Taasisi zote za Umma pamoja
Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Lengo la hatua zinazochukuliwa ni
kuhakikisha kwamba Serikali inasimamia kwa umakini matumizi ya fedha za Umma
ili zitumike ipasavyo kwa malengo yaliyokusudiwa. Hatua hizi zitaimarishwa
zaidi katika mwaka ujao wa fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika,
13.
Kama nilivyoeleza awali hoja
nyingi za msingi zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge kuhusu Mpango wa Taifa,
zimefafanuliwa vizuri na Waheshimiwa Mawaziri wa Kisekta na Mheshimiwa Waziri
wa Fedha na Mipango. Naomba niwaahidi kuwa tutazizingatia katika mchakato wa
maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali ya mwaka 2016/2017, kwa kadri
itakavyowezekana. Waheshimiwa Wabunge watashirikishwa kikamilifu katika
mchakato huo kupitia Kamati mbalimbali za Bunge. Serikali itafarijika sana
kupata maoni na ushauri zaidi ili tuweze kuboresha mipango yetu ya muda mfupi
na muda mrefu.
III:
SEKTA YA KILIMO
Uzalishaji wa Mazao ya Chakula
2014/2015 na Upatikaji wa Chakula 2015/2016
Mheshimiwa Naibu Spika,
14. Hali
ya chakula kwa mwaka 2015/2016 katika maeneo mengi ya nchi imeendelea kuwa ya
kuridhisha kufuatia mavuno mazuri yaliyopatikana msimu wa kilimo wa
2014/2015. Takwimu za Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi zinaonesha kuwa albaki
kutoka msimu uliopita nchi ilikuwa na ziada ya chakula licha ya kuwepo kwa
maeneo machache ambayo hayakuwa na chakula.
Mheshimiwa Naibu Spika,
14.
Kutokana na uzalishaji wa mazao ya chakula kwa msimu wa 2014/2015 kuwa Tani
milioni 15.5 na mahitaji ya chakula kwa mwaka 2015/2016 kuwa Tani milioni
12.9 hivyo nchi imejitosheleza kwa chakula kwa ziada ya Tani
milioni 2.5 sawa na asilimia 120. Napenda kuwahakikishia
Watanzania kuwa Serikali itaendelea kuhudumia maeneo yote yenye uhaba wa
chakula.
Mheshimiwa Naibu Spika,
15. Pamoja
na Taifa kuwa na ziada ya asilimia 120 ya chakula, tathmini ya hali ya
chakula nchini inaonesha kuwa kuna Halmashauri 69 katika mikoa 18 nchini
yenye maeneo yenye dalili za upungufu wa chakula. Maeneo hayo yapo katika
Mikoa ya Dodoma, Shinyanga, Lindi, Singida, Tabora,
Arusha, Geita, Kilimanjaro, Manyara, Mara, Tanga, Simiyu, Mwanza, Morogoro,
Iringa, Njombe, Mtwara, na Pwani.
Mheshimiwa Naibu Spika,
16. Ili
kukabiliana na hali ya uhaba wa chakula katika maeneo hayo, Serikali
inaendelea kutoa chakula katika maeneo hayo ambapo jumla ya Tani 23,871.6 za
chakula zilitengwa kwa ajili hiyo. Hadi kufikia tarehe 17 Januari, 2016,
jumla ya Tani 11,860.8 zilikuwa zimechukuliwa toka Wakala wa Taifa wa
Hifadhi ya Chakula (NFRA) kwenda kwenye Halmashauri za Wilaya zenye upungufu
wa chakula kwa ajili ya usambazaji. Natoa wito kwa Halmashauri ambazo
hazijachukua mgao wao kufanya hivyo mara moja ili Wananchi katika maeneo hayo
wasizidi kuathirika.
Mheshimiwa Naibu Spika,
17. Sambamba na utoaji wa chakula
cha msaada, Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA)
inaendelea kutoa mahindi katika maghala ya Songea na Sumbawanga kwa ajili ya
kuuzwa kwa wafanyabishara wa nafaka walioidhinishwa na mikoa yenye uhaba wa
Chakula. Lengo ni kuongeza upatikanaji wa chakula na kukabiliana na kasi ya
kupanda kwa bei ya vyakula katika maeneo hayo. Chini ya utaratibu huo, vibali
vimeshatolewa kwa wafanyabiashara wa Mikoa 17, vya kununua jumla ya Tani
77,166. Hadi kufikia tarehe 18 Januari, 2016 jumla ya Tani 56,817.5
kati ya Tani 64,817.3 zilizokuwa zimelipiwa kutoka NFRA tayari zilikuwa
zimechukuliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika,
18. Ili kuongeza na kuimarisha
uhakika na usalama wa chakula hapa nchini, Serikali imelenga kujenga maghala 275
kwa awamu katika sehemu zenye uzalishaji mkubwa wa zao la mahindi ambapo hadi
sasa jumla ya maghala 125 yanaendelea kujengwa na kukarabatiwa katika
maeneo hayo. Aidha, Serikali kwa kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya
Chakula (NFRA) inaendelea kujenga maghala ya kimkakati kwa ajili ya kuhifadhi
akiba ya Taifa. Kwa sasa ghala moja lenye uwezo wa kuhifadhi Tani 5,000 limeshajengwa Wilayani Mbozi Mkoani Mbeya. Aidha,
Serikali imepata mkopo wenye masharti nafuu kutoka Serikali ya Poland ambao
utawezesha kujenga vihenge vya kisasa (silos) vyenye uwezo wa
kuhifadhi Tani 160,000 na maghala yenye uwezo wa kuhifadhi Tani 90,000.
Mheshimiwa Naibu Spika,
19. Pamoja
na hatua zinazochukuliwa na Serikali, ninawataka viongozi wa Mikoa, Wilaya na
atendaji katika Halmashauri zote Nchini kuwahamasisha Wananchi kutumia vizuri
mvua zinazonyesha nchini kote kulima kwa bidii ili kuweza kuvuna na kujiwekea
akiba ya chakula cha kutosha kwa ajili ya kaya zao wakati wote wa mwaka.
Aidha, wawahamasishe wafanyabiashara na wadau wengine kusaidia Serikali
kuchukua chakula kutoka maeneo yenye ziada na kupeleka katika maeneo yenye
upungufu. Ni imani yangu kwamba tukizingatia maelekezo haya pamoja na juhudi
za Serikali zilizooneshwa, tatizo la uhaba wa chakula nchini litapungua, kama
siyo kumalizika kabisa.
IV: MIFUGO:
Hatua zilizochukulwa na Serikali
katika Kushughulikia Migogoro ya Wakulima na Wafugaji;
Mheshimiwa Naibu Spika,
20. Migogoro ya ardhi hapa nchini ina sura nne; migogoro kati
ya Wakulima na Wafugaji, mgogoro kati ya Wananchi na Wawekezaji; migogoro
kati ya Wananchi na Serikali na migogoro kati ya Mamlaka moja na Mamlaka
nyingine ndani ya Serikali. Migogoro hii imeenea nchi nzima kutokana na
sababu mbalimbali ikiwepo kuongezeka kwa matumizi ya rasilimali ya ardhi.
21. Serikali
kwa kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa na Tume ya Taifa ya Matumizi
ya Ardhi kwa kutumia Sheria ya Ardhi ya Vijiji Na. 5 ya mwaka 1999 na
Sheria ya matumizi ya Ardhi Na. 6 ya mwaka 2007, hadi kufikia mwezi Juni 2015
jumla ya Vijiji 620 katika Wilaya 81 kwenye Mikoa 22
zimeweza kutenga Hekta Milioni 1.9 kwa ajili ya Wafugaji. Wito wangu
kwa Wananchi na Wadau wa Kilimo na Ufugaji nawaomba kutunza na kuendeleza
maeneo haya ili yaweze kutumika kwa mujibu wa malengo yaliyopangwa.
Mheshimiwa Naibu
Spika,
22.
Nitumie fursa hii pia kulijulisha Bunge lako Tukufu kuhusu hatua ambazo
Serikali imechukua kukabiliana na migogoro ya Wakulima na Wafugaji iliyotokea
katika Mikoa ya Morogoro (Wilaya za Mvomero na Kilombero) na Manyara (Wilaya
ya Kiteto). Katika kushughulikia tatizo hili, Jumla ya Vijiji 53
vimeainisha maeneo kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwemo Kilimo na
Ufugaji. Aidha, jumla ya Mashamba Pori Manane (8) yameanishwa na orodha yake
imewasilishwa kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa
hatua za kufutiwa hati miliki na hatimaye kufanya utaratibu wa kuyatumia kwa
ufugaji. Ni matarajio yangu kuwa maeneo haya yatapunguza sana kwa kiasi
kikubwa matatizo ya uhaba wa malisho hapa Nchini. Wito wangu niwatake
Viongozi wa Vijiji kusimamia vizuri matumizi ya maeneo yatakayotolewa kwa
ajili ya malisho ili tatizo hili la kukosa maeneo ya malisho lisijirudie
tena.
Mheshimiwa
Naibu Spika,
23. Bado
kuna mgogoro wa Wafugaji na Wakulima katika Bonde Oevu la Kilombero ambao
umetafutiwa ufumbuzi kwa kuweka alama (branding) mifugo yote katika
eneo hili ambapo jumla ya Mifugo 52,780 ilipata usajili wa Wilaya.
Aidha, jumla ya Mifugo 24,586 imeondolewa katika eneo la Bonde la
Kilombero. Kwa kuzingatia hatua zilizochukuliwa na Serikali Wananchi
wanapaswa kufuata Sheria na kuhakikisha Mifugo hairudi tena katika maeneo
yaliyokatazwa na kwamba maeneo haya yanahifadhiwa kwa mujibu wa Sheria.
Mheshimiwa
Naibu Spika,
24.
Mgogoro wa Wafugaji na Wakulima katika maeneo ya Kiteto ni wa muda mrefu na
kwa bahati mbaya sana umeleta madhara makubwa kwa maisha ya Wanadamu na
uharibifu wa mali. Napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba Tume
iliyoundwa na aliyekuwa Waziri Mkuu (Mstaafu) Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda
ikiongozwa na Askofu Amos Mhagachi imekamilisha hatua muhimu ya kuleta
maelewanao na maridhiano katika pande zilizoathirika na mgogoro huo. Kwa sasa
hali imeendelea kuimarika na tunaendelea kufuatilia kuhakikisha inakuwa
shwari kwa muda wote.
25.
Vilevile tarehe 29 Januari 2016 nimekutana na Viongozi wa Serikali,
Halmashauri ya Wilaya na Chama kutoka Wilaya ya Kiteto hapa Dodoma ambapo
nilipata fursa ya kupokea taarifa ya Tume niliyoitaja hivi punde. Nimeiagiza
Tume kuendelea na hatua iliyobakia ili kurejesha utulivu na amani kwa
wananchi wa Kiteto. Hata hivyo, nimepanga kufanya ziara Wilayani Kiteto
katika siku chanche zijazo ili niweze kukutana na Wananchi walioathirika na
mgogoro huu na ikiwa ni pamoja na kujionea hali halisi Wilayani Kiteto ili
tuweze kutatua migogoro yote. Wito wangu kwa ndugu zangu wa Kiteto ni
kuwaomba waendelee kuvumilia wakati jitihada za Serikali katika kutatua
migogoro hiyo inaendelea.
V:
UTEKELEZAJI WA ELIMU MSINGI BILA MALIPO
Mheshimiwa
Naibu Spika,
26. Tangu
Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli atoe maaelezo ya utekelezaji wa
elimu ya msingi bila malipo, kumekuwa na umuhimu wa kutoa elimu na ufafanuzi
zaidi juu ya utekelezaji wa agizo la elemu bila malipo kwa Watanzania kuanzia
darasa la awali hadi Kidato cha Nne katika Shule za Umma. Hii ni hatua ya
Serikali katika kuhakikisha uwepo wa fursa ya elimu bora kwa wote kwa
kuwapunguzia mzigo wazazi na walezi kugharamia au kuchangia upatikanaji wa
elimumsingi.
Katika mpango huu, Serikali
imedhamiria kuhakikisha kuwa mwanafunzi atasoma kuanzia darasa la awali hadi
kidato cha Nne bila ya wazazi na walezi kulipa ada ya shule, gharama za
mitihani na michango mbalimbali. Hata hivyo, yapo majukumu ambayo yataendelea
kutekelezwa na wazazi na walezi wote ambayo ni pamoja na kununua sare za
shule na michezo, madaftari, kalamu na chakula kwa wanafunzi wa shule za
kutwa zilizojiwekea utaratibu huo. Maeneo mengine ni kulipia nauli ya kwenda
na kurudi shule, na mahitaji mengine kama kununua godoro, shuka na vifaa vya
usafi binafsi. Mzazi au mlezi anao wajibu wa kugharamia matibabu ya mtoto
wake.
Mheshimiwa Naibu Spika,
27.
Napenda nitumie nafasi hii kuwaomba Waheshimiwa Wabunge wote tushirikiane
katika juhudi za kuunga mkono uamuzi wa Serikali kuhusu elimu bila malipo.
Aidha, nawaomba wote kwa ujumla wetu kushirikiana kuwaelimisha Wananchi wetu
kuhusu utaratibu huu na wajibu wa kila mmoja wetu kama Mzazi/Mlezi, Serikali
na jamii kuhusu utekelezaji wa zoezi hili. Nia yetu ni kuhakikisha kwamba
Watanzania wanapata fursa ya kupata elimu bora kwa mtoto mwenye umri wa
kwenda Shule na wote walioko katika Shule za Msingi na Sekondari. Napenda pia
kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba kama tulivyokwisha sema suala la ada
elekezi inafanyiwa kazi na ikikamilika Wananchi watajulishwa kuhusu utaratibu
huo. Vikao vya pamoja baina ya Serikali na wadau vitaanza hivi karibuni.
Mheshimiwa Naibu Spika;
28. Katika
kutekeleza mpango huu, Serikali imetenga fedha shilingi Bilioni 131.4
kuanzia mwezi Disemba 2015 hadi Juni, 2016, kuhudumia wanafunzi wa bweni kwa
chakula, kufidia gharama za ada za mitihani, ada ya shule na kutoa fedha za
uendeshaji wa shule (Capitation Grants). Aidha, kupitia Waraka
wa Elimu Na. 5 wa mwaka 2015, Serikali imefuta michango yote iliyokuwa
inachangishwa shuleni kwa idhini ya Kamati na Bodi za Shule.
Mheshimiwa Naibu Spika,
29.
Tunatambua katika utekelezaji wa zoezi hili zipo changamoto zilizojitokeza.
Kwa mfano, baadhi ya shule zenye wanafunzi wachache kupata fedha kidogo sana
kwa kuwa ugawaji wa fedha unazingatia idadi ya wanafunzi. Lakini pia zipo
changamoto katika kutoa chakula cha mchana kwa wanafunzi wa kutwa na
uendeshaji wa Hosteli ambazo wazazi na walezi au jamii walikuwa wanachangia
fedha za chakula. Serikali inaendelea kuzifanyia kazi changamoto hizo
zilizojitokeza katika utekelezaji wa mpango huu ikiwemo uelewa wa jamii na
wadau kuhusu mpango mzima kwa ujumla wake.
VI: HUDUMA YA MIKOPO KWA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU
Mheshimiwa Naibu Spika,
30.
Serikali imeendelea kutoa huduma ya mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa
mwaka wa masomo 2015/2016 kwa kuzingatia Sheria ya Bodi ya Mikopo ya
Wanafunzi wa Elimu ya Juu Namba 9 ya mwaka 2004 (Kama ilivyorekebishwa),
Kanuni za Utoaji Mikopo za mwaka 2008, na Mwongozo wa utoaji Mikopo na Ruzuku
kwa mwaka wa masomo 2015/2016. Hadi kufikia mwishoni mwa Januari 2016,
Serikali ilikuwa imetoa mikopo yenye thamani ya Shilingi Bilioni 207.9
kwa wanafunzi 122,786 wa elimu ya juu, wakiwemo wanafunzi wa mwaka wa
kwanza 53,850 ambao ni asilimia 98.9 ya wanafunzi 55,254
walioomba mikopo hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika,
31. Ili
Taifa liendelee kuwa na wataalamu wa kutosha katika nyanja muhimu, Serikali
itaendelea kutoa kipaumbele cha kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu
wanaodahiliwa katika programu za kipaumbele ikiwemo Sayansi
za Tiba, Ualimu wa Sayansi na Hesabu, Uhandisi wa Mafuta na Gesi, Uhandisi
Umwagiliaji, Sayansi za Kilimo, Wanyama na Ardhi. Aidha, Serikali inaendelea
kufanyia kazi mikakati ya kuimarisha urejeshaji wa mikopo pamoja na kuwa na
vyanzo endelevu vya kupata fedha za kumudu ongezeko la wanafunzi wenye
mahitaji ya mikopo.
VII:
HALI YA USALAMA NCHINI
Mheshimiwa Naibu Spika,
32. Hali ya usalama katika Nchi yetu kwa ujumla ni
shwari. Hata hivyo, katika kipindi hiki nchi yetu
imekuwa ikikabiliana na changamoto ya ongezeko kubwa la Wakimbizi
hususan katika Mkoa wa Kigoma. Kambi zetu zilizoko mikoa ya Kigoma, Katavi,
Tabora na Tanga zinahifadhi wakimbizi wapatao 218,895 kutoka
mataifa ya Burundi (wakimbizi 156,377),
Congo-DRC (wakimbizi 62,176), Somalia (wakimbizi 150) na
Mataifa Mchanganyiko (wakimbizi 192) kutoka nchi za Rwanda, Uganda,
Sudan ya Kusini na Ethiopia. Kwa ujumla, katika kipindi hiki wamepokelewa
wakimbizi zaidi ya 122,267 kutoka Burundi. Aidha, hadi kufikia
tarehe 31 Desemba, 2015 kambi mpya ya wakimbizi ya Nduta
imepokea wakimbizi 38,994 wengi kati yao
wamehamishiwa kutoka Kambi ya Nyarugusu na wachache wakiwa wameingia moja kwa
moja kutokea Burundi.
Mheshimiwa Naibu Spika,
33.
Kufuatia ujio wa wimbi kubwa la wakimbizi toka Burundi kumejitokeza matukio
ya uhalifu wa kutumia silaha za moto ndani na nje ya kambi ya wakimbizi ya
Nyarugusu. Aidha, kutokana na upekuzi na ukaguzi
kwa wakimbizi unaofanywa kwa pamoja na vyombo vya dola sanjari na
taarifa za ki-intelijensia imebainika kuwepo kwa askari waasi waliokimbia
pamoja na raia wa kawaida ambao wanajaribu kuwashawishi vijana kujisajili ili
kujiunga na vikundi vya waasi. Nitoe wito kwa wananchi na wakimbizi
kushirikiana na vyombo vyetu vya usalama kwa kutoa taarifa za uhalifu,
hususan umiliki haramu wa silaha za moto kwenye makambi na katika maeneo
mbalimbali.
VIII:
MPANGO ENDELEVU WA USAFI WA MAZINGIRA NCHNI
Mheshimiwa Naibu Spika,
34.
Mtakumbuka kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, aliamua maadhimisho
ya miaka 54 ya Uhuru ya terehe 9 Desemba, 2015 yafanyike kwa kufanya usafi wa
mazingira katika maeneo ya Umma na maeneo yanayowazunguka. Kwa ujumla Wananchi,
Taasisi za Umma na Binafsi ziliitikia agizo hilo na kushiriki kikamilifu
katika zoezi hilo. Nichukue fursa hii kuwapongeza kwa dhati wananchi, taasisi
za umma na binafsi wote kwa kushiriki katika zoezi hilo kikamilifu. Mlionesha
moyo wa uzalendo na ari kwa nchi yenu. Nawapongeza sana!
Mheshimiwa Naibu Spika,
35. Usafi
ni dhana muhimu katika kulinda afya za binadamu na kudhibiti magonjwa
mbalimbali ya mlipuko ikiwemo kipindupindu. Ili kufanikisha lengo hili,
kunahitajika juhudi za makusudi na za pamoja katika usimamizi wa sheria,
kanuni na taratibu tulizojiwekea. Hivyo, Serikali imeamua kulifanya zoezi la
usafi wa mazingira kuwa endelevu. Kupitia Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Serikali
imetoa Waraka unaoelekeza kuwa kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi iwe Siku
Maalum ya kufanya Usafi wa Mazingira.
Mheshimiwa Naibu Spika,
36.
Napenda kuendelea kusisitiza katika kila ngazi yaani Viongozi na Wananchi
kutimiza wajibu wao kwa kuhakikisha zoezi hili linakuwa endelevu. Aidha,
napenda kuwahimiza Viongozi wa Mkoa, Wilaya na Halmashauri kusimamia usafi wa
mazingira katika maeneo yao ya utawala zoezi ambalo litakuwa linafanyika kila
Jumamosi ya mwisho wa mwezi. Kila Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya nchini
awe na mikakati ya kudumu ya usafi ikiwa ni pamoja kuhakikisha kuwa kuna
sheria ndogo za usafi wa mazingira na zinatekelezwa ipasavyo. Aidha,
Halmashauri zote nchini zihakikishe kuwa uchafu uliokusanywa katika maeneo
mbalimbali unazolewa na kupelekwa katika maeneo mahususi ya dampo. Simamieni
kikamilifu wakandarasi waliopewa zabuni hizo na kuona wanatimiza wajibu wao
kikamilifu.
Mheshimiwa Naibu Spika,
37. Kama
tulivyoona Usafi wa mazingira ni jukumu la kila Mwananchi na linapaswa kuwa
endelevu. Rai yangu kwa Watanzania wote ni kujenga tabia ya kuhakikisha kuwa
mahali pa kazi na mazingira yanayowazunguka yanakuwa safi wakati wote.
Kufanya hivyo, kutasaidia kuimarisha usafi wa mazingira na kuboresha afya.
Hali kadhalika kupunguza mlipuko wa magonjwa yakiwemo kipindupindu.
38. Wito
wangu kwa Wananchi ni kuona kuwa zoezi la usafi ni la kila mmoja wetu na
kuepuka kuchafua mazingira kwa makusudi ikiwemo kuepuka tabia za kutupa taka
hovyo wanapokuwa katika vyombo vya usafiri na pia kutofanya biashara katika
maeneo yasiyoruhusiwa ili kuzuia kutupwa taka hovyo. Wamiliki wa mabasi
yanayofanya safari ndefu wanatakiwa waweke vifaa vya takataka. Yeyote
atakayebainika kutupa takataka dirishani, atachukuliwa hatua za kinidhamu
ikiwa ni pamoja na mmiliki wa basi hilo.
Watendaji wa Mitaa na Kata na
Vijiji kutimiza wajibu wao wa kuhakikisha maeneo wanayoyasimamia yanakuwa
katika hali ya usafi. Nitumie fursa hii kuwahimiza Wananchi, Taasisi na
Jumuiya zote kuhakikisha wanaweka mazingira katika hali ya usafi na pia
kushiriki katika siku ya usafi kama iliyopangwa na Serikali.
IX: UHUSIANO
WA KIMATAIFA
Mheshimiwa
Naibu Spika,
39. Nchi
yetu imeendelea kuwa kivutio kikubwa katika mahusiano baina ya Nchi na Nchi,
Jumuiya za Kikanda na Kimataifa. Hii inatokana na Viongozi wetu ambao
wamekuwa katika mstari wa mbele kudumisha mahusiano yetu katika Medani za Kimataifa.
Yapo mambo mengi yaliyofanyika na yanayo endelea kufanyika kama mwendelezo wa
kudumisha ushirikiano katika Jumuia hizi za Kikanda na Kimataifa.
Mheshimiwa
Naibu Spika,
40.
Kutokana na juhudi za Viongozi wetu kutangaza Nchi yetu Kimataifa, ni hivi
karibuni tu Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu
ya Nne ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja
wa Mataifa, Bwana Ban Ki-moon kuwa mmoja wa Wenyeviti wa jopo la ushauri la
ngazi ya juu kuhusu Afya ya Mama na Mtoto Duniani (Every Woman, Every
Child). Hii ni heshima kubwa kwa nchi yetu kwa kuwa itaiweka Tanzania
kuwa miongoni mwa mataifa yenye kuheshimika duniani. Aidha, uteuzi huu ni
chachu ambayo inaleta matumaini mapya katika kukabiliana na changamoto za
afya ya mama na mtoto, hususan katika nchi zinazoendelea kama Tanzania.
Nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa
uteuzi huo. Tunamuombea heri na baraka tele katika kutekeleza jukumu hilo
kubwa la Kimataifa kwa maendeleo ya watu wetu.
X:
KUIMARISHA UTENDAJI SERIKALINI NA MAADILI
Mheshimiwa
Naibu Spika,
41.
Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi imedhamiria
kurejesha nidhamu na maadili ya Watendaji wa Serikali na Watumishi wa Umma
katika kutoa huduma mbalimbali kwa Wananchi kwenye maeneo mbalimbali. Katika
kuhakikisha Watumishi wa Umma na Watanzania wote wanafanya kazi, Mheshimiwa
Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amekuja na
kauli mbiu ya “Hapa Kazi Tu”. Tafsiri ya falsafa hii ni kuwataka
Watanzania wote katika nafasi mbalimbali walizopo kufanya kazi kwa bidii na
kujiepusha na vitendo vya uzembe, urasimu na kutenda kazi kwa mazoea.
42. Aidha, Katiba
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 chini ya Ibara ya 22
inaainisha kuwa, kila Mtu anayo haki ya kufanya kazi. Vilevile, Ibara
ya 25 inafafanua kuwa kufanya kazi ndiyo njia pekee ya kumwezesha
Mtanzania kupata utajiri na ndilo chimbuko la ustawi wa wananchi na ni kipimo
cha utu.
Wakati akihutubia Mkutano wa
kwanza wa Bunge lako Tukufu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, kwa maneno
yake alisema, napenda kunukuu:-
“Serikali nitakayounda, nataka iwe
inawahudumia Wananchi kwa haraka na sio kuwasumbua sumbua na kuwazungusha.
Natoa rai kwa Watumishi wa Serikali, hasa ambao ni wazembe na wavivu,
kujiandaa. Wamevumiliwa kwa muda mrefu sasa basi. Kwa sababu Watumishi wa
aina hiyo hawatavumiliwa katika Serikali nitakayoiongoza. Lugha za “Hiyo
ni changamoto tutaishughulikia” au “Mchakato unaendelea” hazitavumiliwa
katika Serikali ya Awamu ya Tano. Mimi nataka watu wa Kazi tu.
Hatuwezi kulea watu ambao wanalipwa mishahara lakini hawafanyi kazi
wanazotakiwa kufanya, au wamegeuza Ofisi za Umma kuwa ni mahala pa kuchuma
bila kufanya kazi.” mwisho wa kunukuu.
Mheshimiwa Naibu Spika,
43.
Ili kutekeleza maneno ya Mheshimiwa
Rais na kuhimiza matakwa ya Kikatiba, kila Mtanzania anapaswa kushiriki na
kujituma kwa uaminifu katika kazi halali za uzalishaji mali. Aidha, kila
Mwananchi anapaswa kuwa na nidhamu ya kazi na kuhakikisha anafikia malengo yaliyowekwa.
Nitumie fursa hii pia kuwakumbusha Watumishi wa Umma kuwa wamepewa dhamana ya
kuwahudumia Wananchi kwa niaba ya Serikali. Hivyo wanawajibika kuhakikisha
wanawahudumia Wananchi kwa haki, weledi, uadilifu na kwa taaluma zao. Ni
lazima wahakikishe kuwa wanatatua kero za Wananchi. Sio sahihi wananchi
kuwasilisha kero zao kwa viongozi wa ngazi za kitaifa hasa wakati wa ziara
ilhali viongozi wa mikoa na wilaya wapo katika maeneo hayo kwa wakati wote.
44.
Tunatambua kuwa wapo Watumishi wanaotekeleza vyema majukumu
yao. Lakini pia wapo Watumishi ambao hawazingatii maadili ya kazi zao na pia
wanafanya kazi kwa uzembe. Serikali haitaacha kuchukua hatua za nidhamu kwa
watumishi wote wasiozingatia kikamilifu sheria, kanuni na taratibu katika Utumishi
wa Umma. Aidha, kwa kuzingatia maelekezo ya
Mheshimiwa Rais, Viongozi na Watumishi wote wa Umma lazima tufanye kazi kwa
kuzingatia weledi na kujiamini. Kila mtu anapaswa kujitathmini kama dhamana
aliyopewa anaitendea haki.
Mheshimiwa Naibu Spika,
45.
Huu sasa ni wakati wa kufanya
mabadiliko ya dhati katika utendaji na uadilifu. Kwa maana hiyo napenda
kusisitiza mambo yafuatayo kwamba:-
(i) Kila Kiongozi na Mamlaka ya nidhamu ni lazima
kuwajibika kusimamia Utendaji na Maadili ya Kazi. Hatua za kinidhamu
zichukuliwe kwa wakati na kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za
utumishi. TUSIONE HAYA HATA MARA MOJA, CHUKUENI HATUA.
(ii) Wananchi wahudumiwe ipasavyo na kwa weledi,
haki, uadilifu na heshima. Mambo haya yakizingatiwa hakuna mwananchi
atakayesafiri kutoka kijijini, wilayani au mkoani kutafuta huduma Makao Makuu
ya Wizara, Ofisi ya Waziri Mkuu au IKULU.
(iii) Madawati ya malalamiko yawepo katika Ofisi za
Umma. Aidha, tayari maelekezo yametolewa ya Watumishi wa Umma wazingatie
utaratibu wa kuvaa vitambulisho vyenye majina yao kwa urahisi wa wananchi
kuwatambua wanapowahudumia. AGIZO HILI LITEKELEZWE.
Mheshimiwa Naibu Spika,
46.
Ni kweli kwamba, Mheshimiwa Rais
ametumia dhana ya “kutumbua jipu” kama dawa ya kusimamia uwajibikaji
hasa katika wale wenye dalili ya kukosa maadili ya Utumishi wa Umma. Tafsiri
ya dhana hii ya “Kutumbua jipu” inalenga katika kuwarejesha Watumishi
wa Umma na walioko Serikalini katika mstari mzuri wa utendaji. Nitoe wito kwa
Waheshimiwa Wabunge wote kama tulivyo na kwa umoja wetu, tumuunge mkono
Mheshimiwa Rais katika vita hii kubwa ya “Kutumbua Majipu”.
Tukiwa pamoja na kwa kushirikiana tutaweza kuibadilisha nchi yetu kuwa
nchi ya maadili na yenye sifa ya juu katika utendaji wa Utumishi wa Umma.
Mheshimiwa
Naibu Spika,
47.
Aidha,
naomba nisisitize kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ya Mheshimiwa Dkt. John
Pombe Magufuli inaongozwa na Katiba, Sheria, Kanuni na Taratibu za Nchi.
Vilevile inaheshimu na kuthamini haki za Watumishi wa Umma wa ngazi zote na
inatambua mchango mkubwa unaotolewa na Watumishi wa Umma katika kuchangia
ukuaji wa uchumi wa Taifa. Kamwe, Serikali haitamwonea mtumishi yeyote wala
kumnyanyasa endapo tu atakuwa anatenda yale yanayopasa. Lakini pia haitamvumilia
mtumishi mzembe na asiyetimiza wajibu wake. Serikali itaendelea kuchukua
hatua za kurejesha nidhamu kwa Watumishi wa Umma ili kuwezesha Nchi yetu kuwa
na Utumishi wenye kuzingatia uadilifu na uliotukuka.
XI:
HITIMISHO.
Mheshimiwa
Naibu Spika,
48.
Uzoefu nilioupata katika muda
mfupi tuliokaa pamoja hapa Bungeni, nimegundua kuwa tuna Waheshimiwa Wabunge
mahiri waliobobea katika nyanja mbalimbali. Wapo wasomi wa ngazi zote, wazee
kwa vijana ambao wana uzoefu na utaalam mkubwa. Ni imani yangu kuwa tutatumia
utaalam na uwezo mkubwa tulionao katika kuijenga nchi yetu na kuwasaidia
Watanzania kutoka hapa tulipo hadi hatua ya mbele katika kuleta maendeleo.
Wananchi waliotuchagua wanatutegemea. Nawaomba tutangulize uzalendo katika
kila jambo tufanyalo kwa manufaa ya Taifa letu na watu wake. Tufike mahali
ambapo kwa elimu, busara na hekima tulizonazo kuacha kabisa ushabiki wa
kisiasa badala yake tutizame mbele katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Mheshimiwa
Naibu Spika,
49.
Napenda kuhitimisha Hotuba yangu
kwa kurejea tena nilivyosema hapo awali kwamba, baada ya kukamilika kwa
Uchaguzi Mkuu kwa mafanikio makubwa, kazi kubwa iliyo mbele yetu ni kuijenga
nchi yetu kwa umoja na mshikamano. Nawaomba tuweke maslahi ya Watanzania na
Taifa letu mbele. Tudumishe amani na utulivu. Tupuuze sera zozote za
kudhoofisha utaifa wetu kama Watanzania na kutugawa kwa misingi yoyote ile,
iwe ya kikabila, imani za dini, rangi au kwa itikadi za kisiasa. Dhamira yetu
sote iwe ni kukuza uchumi wa nchi yetu na kuondoa umaskini ili kuwaletea
wananchi wetu maendeleo na maisha mazuri.
50.
Ni jukumu la kila mmoja wetu
kuhakikisha kuwa Tanzania inapiga hatua mbele. Tufanye kazi kwa bidii kuunga
mkono kaulimbiu yetu ya “Hapa ni Kazi Tu”. Aidha tutumie juhudi,
maarifa na ubunifu zaidi katika kila jambo. Mimi naamini kuwa kwa ushirikiano
katika Bunge hili na wananchi kwa ujumla, tutaweza kutimiza matarajio ya
wananchi waliotuchagua na matarajio ya Watanzania wote.
Mheshimiwa
Naibu Spika,
51. Naomba nitumie nafasi hii tena kuwashukuru wote
waliosaidia kufanikisha mkutano huu. Nikushukuru wewe Naibu Spika, na
Mheshimiwa Spika kwa kutuongoza vizuri na kwa weledi mkubwa. Kipekee
niwashukuru Wenyeviti wa Bunge ambao wamekalia kiti kwa mara ya kwanza lakini
kwa weledi mkubwa, Hongereni sana!!.
Mheshimiwa Naibu Spika,
52. Nitumie nafasi hii kumshukuru Katibu wa Bunge na Wasaidizi
wake wote kwa kazi nzuri ya kuhakikisha mkutano huu unakamilisha shughuli
zake kama ilivyopangwa. Niwashukuru Wataalam wote wakiwemo Waandishi wa
Habari kwa kazi nzuri waliyofanya kufanikisha Mkutano huu.
Mheshimiwa Naibu Spika,
53. Nimalizie kwa kuwatakia wote safari njema mnaporejea
kwenye maeneo yenu ya kazi na katika majimbo yenu. Ninaamini kwamba,
Mwenyezi Mungu atatulinda na kutuweka salama sote kama tulivyo hadi kukutana
tena katika Mkutano ujao.
Mheshimiwa Naibu Spika,
54. Baada ya kusema hayo, naomba sasa kutoa Hoja kwamba, Bunge
lako Tukufu liahirishwe hadi tarehe 19 Aprili, 2016 saa 3:00
asubuhi litakapokutana katika Mkutano wa Tatu kwenye Ukumbi huu hapa
Dodoma.
Mheshimiwa Naibu Spika,
55. Naomba kutoa Hoja.
Asante
kwa kuendelea kufuatilia P5 TANZANIA MEDIA kwa habari motomoto
|
Comments