CHENJI YA SHILINGI 500/=MKAZI SUMBAWANGA AHUKUMIWA MIAKA 10 KWA KUUA BILA KUKUSUDIA.
Na.Issack Gerald-Sumbawanga
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Sumbawanga mkoani Rukwa imemhukumu
kifungo cha miaka 10, mkazi wa kijiji cha Kazila Lizberth Fredinad (21) baada
ya kupatikana na hatia ya kumuua Charles Abel bila kukusudia.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa Fredinad alimuua Charles Abel
kwa kumchoma na kuni tumboni akigoma kumlipa marehermu chenji yake ya shilingi
500 aliyokuwa akidaiwa.
Akisoma hukumu hiyo jana, Jaji Mfawidhi Kakusulo Sambo
alisema kuwa anatoa adhabu hiyo kali kwa mshtakiwa huyo ili iwe fundisho kwake
na wengine wenye tabia ya kujichukulia sheria mkononi.
Awali Mwendesha Mashtaka, wakili wa serikali Happiness
Mayunga alidai mahakamani hapo kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo Februari
6, mwaka jana na kusababisha kifo.
Ilidaiwa kuwa siku hiyo ya tukio, mshtakiwa huyo aliingia
katika kilabu cha pombe za kienyeji ambapo pia palikuwa panachomwa nyama ya
nguruwe na kukuta wateja wengine wawili wakinywa pombe hiyo.
Ilielezwa kuwa ndipo marehemu alipoanza kumdai marehemu ampe
chenji yake ya shilingi 500 na kusababisha ugomvi kuibuka baina yao na kuanza
kupigana.
Kwa mujibu wa Wakili Mayunga ugomvi huo uliodumu kwa muda
mrefu kila wakisuluhishwa waliendelea kupigana ndipo mstakiwa alipomchoma tumbo
Charles kwa kuni na kumjeruhi vibaya ambapo alikimbizwa katika zahanati
kijijini Kaengesa, Manispaa ya Sumbawanga kwa matibabu.
Comments