RIPOTI YA KUKAMATWA KWA WATUHUMIWA WA NYARA ZA SERIKALI KATAVI HII HAPA KUANZIA DESEMBA 24,2014--DESEMBA 30,2015
Na.Issack Gerald-Katavi
JESHI la Polisi
mkoani Katavi kwa kushirikiana na askari wa Shirika la Hifadhi za Taifa
(TANAPA), wamefanikisha kukamata watu 11 wanaohutumiwa kumiliki nyara za
serikali, yakiwemo meno ya tembo yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 532.5
kati ya Desemba 24, 2014 na Desemba 30 mwaka 2015.
Kamanda wa polisi Mkoani Katavi Dhahiri Kidavashari (PICHA na Issack Gerald) |
Kwa mujibu wa
Kamanda wa Polisi mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari, katika kipindi hicho
vipande 67 vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilo 155.5 vilikamatwa, vyote
vikiwa na thamani ya sh milioni 515.5.
Alisema watuhumiwa
saba kati ya 11 wameshafikishwa mahakamani ambapo wengine wanatumikia vifungo
huku mashauri ya wengine yakiwa katika hatua mbalimbali za kusikilizwa.
Watuhumiwa watatu wanaendelea kuhojiwa ambapo watafikishwa mahakamani mara tu
baada ya upelelezi wa awali wa shauri lao kukamilika.
Alisema kati ya
Desemba 24 mwaka 2014 na Januari 12 mwaka 2015 watuhumiwa wanne wanaosadikiwa
wanamtandao wa biashara haramu ya meno ya tembo walikamatwa wakituhumiwa
kukutwa na vipande 47 vya meno ya tembo vikiwa na uzito wa kilo 88.7 vyenye
thamani ya zaidi ya Sh milioni 306 .
Aidha, Desemba 24
mwaka 2014 saa kumi na mbili alfajiri Jeshi la Polisi mkoani humo liliwakamata
watu wawili mjini Mpanda wakiwa wanataka kusafirisha vipande 22 vya meno ya
tembo nyenye uzito wa kilo 46.3 vyenye thamani ya zaidi ya milioni 157 katika
basi la Adventure.
Akizungumza na
gazeti hili kwa njia ya simu Kamanda Kidavashari alisema Januari 12, mwaka 2015
, saa mbili na robo usiku watuhumiwa wengine wawili walikamatwa wakiwa na
vipande 25 vya meno ya tembo vikiwa na uzito wa kilo 42 vyenye thamani ya zaidi
ya Sh milioni 148.5.
Akifafanua,
alisema watuhumiwa hao walikamatwa na askari polisi wawili waliokuwa walisindikiza
basi la abiria, mali ya Kampuni ya AM yenye namba za usajili T 740 AQD
lililokuwa likitokea mjini Mpanda mkoani humo na kuelekea Mwanza. “Watuhumiwa
hao walikamatwa baada ya kutiliwa mashaka na askari polisi walipokuwa wakipanda
basi hilo la abiria wakiwa na mabegi matatu waliyoingia nayo ndani ya gari
hilo,“ alieleza.
Aprili 4 mwaka
2015, Polisi mkoani Katavi iliwakamatwa na watu wawili wakituhumiwa kukutwa na
nyara ya Serikali yenye thamani ya zaidi ya Sh 49.5. Nyara hizo za Serikali
zimetambuliwa kuwa ni vipande vinane vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilo
8.2.
Alisema watuhumiwa
hao walikamatwa Aprili 04, mwaka 2015 , saa sita usiku katika wakiwa katika
nyumba ya kulala wageni iitwayo Salama iliyopo katika eneo la Majengo mjini
Mpanda.
“Kabla ya
watuhumiwa kukamatwa, Jeshi la Polisi lilipata taarifa za kiitelijensia kutoka
kwa raia mwema kuwa katika nyumba ya kulala wageni ya Salama kuna wageni wawili
wana meno ya tembo … mtego uliwekwa na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa,”
alisisitiza.
Jeshi la Polisi
mkoani Katavi liliendelea kupata mafaniko makubwa katika mapambano dhidi ya
ujangili baada ya kuwakamata watu wawili wakiwa na vipande nne vya meno ya
tembo vyenye uzito wa kilogramu 47.6 vyenye ya zaidi ya Sh milioni 60 .
Kwa mujibu wa
Kidavashari walikamatwa Novemba 11 mwaka 2015 saa saba na nusu mchana katika
kitongoji cha Tompola kijiji cha Usevya, tarafa ya Mpimbwe wilayani Mlele.
Kutokana na matukio hayo, Kamanda Kidavashari ameendelea kuonya wananchi
kuachana na biashara haramu za nyara za serikali na uwindaji haramu kwani ni
uharibifu wa rasilimali za Taifa.
Comments