MARUFUKU VITUO VYA POLISI KUCHOMWA MOTO
JESHI la Polisi Mkoa wa Morogoro limekaririwa likisema linawashikilia watu 11 kwa tuhuma za kuchoma kituo kidogo cha Polisi kilichopo Mofu wilayani Kilombero baada ya kukivamia kwa lengo la kutaka polisi wawape mtuhumiwa wa mauaji ili wamuue.
IGP ERNEST MANGU |
Tukio la kuchomwa kwa kituo hicho limetokea ikiwa ni siku chache baada ya wananchi wenye hasira kuvamia Kituo cha Polisi Bunju A kilichopo Dar es Salaam na kukichoma moto kwa kile kilichoelezwa ni dereva kumgonga mwanafunzi na kupoteza maisha.
Tuseme tu hapa kuwa utamaduni huu wa kuchoma vituo vya Polisi ni lazima ukomeshwe kwa sababu si suluhu la wananchi kupata kile wanachodai zaidi ya kuisababishia Serikali hasara na wakati huo huo kukwamisha huduma nyingine za kijamii.
Kama kuna tatizo limetokea ni kufuata taratibu na si kukimbilia kuchoma vituo vya polisi au taasisi nyingine za serikali au binafsi. Hatutakiwi kufumbia macho vitendo vya aina hiyo kwa sababu havijengi zaidi ya kuharibu.
Pia, hatuungi mkono watu wanaovunja sheria iwe kwa kusababisha ajali au kufanya mauaji. Wanaofanya hivyo lazima sheria ichukue mkondo wake. Kama ni dereva ni lazima awe makini barabarani na kuheshimu vivuko vya watembea kwa miguu.
Ni lazima kutii sheria bila shuruti kama Jeshi la Polisi linavyosema. Ni lazima kuishi kwa misingi ya haki na utawala bora, vinginevyo kila kitu kinatakwenda ovyo ovyo. Kwa msingi huo ni jambo jema kila mmoja wetu kuzingatia taratibu zilizopo.
Kama tutajenga vituo vya Polisi kwa gharama kubwa halafu baadhi ya watu wanavivunja au kuchoma moto kama inavyotokea hatukomoi mtu bali sisi wenyewe. Hii ni kwa sababu vituo hivyo vinajengwa kwa kodi zetu au jasho letu.
Ni matarajio yetu kuwa kila mwananchi atajitahidi kufuata sheria katika kutafuta haki na si kuchukua hatua ambazo hazijengi zaidi ya kubomoa.
Chanzo :Jambo leo
Comments