ASASI ZA KIRAIA ZAINGILIA KATI SUALA LA KUONDOLEWA WALIMU WA ELIMU MAALUMU SHULENI AZIMIO
Asasi za kiraia Mkoani Katavi
zimelazimika kufika katika Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya
Manispaa ya Mpanda Mkoani Katavi ili kuzungumza naye kuhusu hatua ya kuwaondoa
walimu waliokuwa wakifundisha watoto wenye ulemavu katika Shule ya Msingi
Azimio bila kuweka wengine mbadala.
Asasi hizo zimesema katika kipindi
cha mwaka 2015 mpaka sasa wanafunzi wenye ulemavu hawafundishwi masomo
inavyotakiwa baada ya walimu watatu kati ya watano wa elimu maalumu waliokuwepo
kuondolewa katika shule hiyo na kupangiwa majukumu mengine.
Zimesema,walimu watatu walioondolewa
shuleni walipandishwa madaraja kuwa walimu wakuu katika shule zisizokuwa na
watoto wenye ulemavu,mwingine akipandishwa daraja na kuwa mratibu elimu maalumu
katika Manispaa ya Mpanda ambapo mpaka sasa amebaki mwalimu mmoja anayefundisha
darasa la kwanza mpaka la saba.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji
wa Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda Bw.Michael Nzyungu amesema hakuwa na
taarifa ya kuondolewa kwa walimu hao na amemwagiza Afisa elimu wa Manispaa ya
Mpanda kuchukua hatua za haraka ili mpaka kufikia wiki ijayo liwe limepatiwa
ufumbuzi.
Shule ya Msingi Azimio yenye
wanafunzi 20 wenye ulemavu kuanzia darasa la kwanza Mpaka la Saba,ina wanafunzi
3 wa darasa la saba na 3 wa darasa la nne wanaotarajia kufanya mtihani mwishoni
mwa mwaka huu.
Baadhi ya asasi zilizofika katika
Ofisi ya Mkurugenzi ni pamoja na Waratibu wa mradi wa elimu Jumuishi Mkoani
Katavi, Shirikisho la vyama vya watu wenye Ulemavu SHIVYAWATA na wajumbe wa
kamati ya kulea baraza la watoto wenye ulemavu Wilayani Mpanda.
HABARI ZAIDI NA P5TANZANIA LIMITED
Comments