HIVI TANZANIA TUNAKOELEKEA NI WAPI?KIONGOZI WA WANAFUNZI TANZANIA ABDUL NONDO NAYE ATOWEKA


Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP) umesema mwenyekiti wake Mahmud Abdul Ormari Nondo hajulikani alipo na kulitaka jeshi la polisi kuhakikisha anapatikana akiwa salama kwa haraka.

Baba mdogo wa kiongozi huyo Mussa Mitumba akiwahutubia wanahabari pia ametoa wito kwa 'mwanawe' kurudishwa akiwa hai aendelee na kutafuta kutimiza ndoto zake.
Abdul Nondo alituma ujumbe wa mwisho kusema alikuwa hatarini

Kiongozi huyo wa wanafunzi alionekana mara ya mwisho mnamo Jumanne katika afisi za shirika hilo eneo la Sinza, Dar es Salaam alipokuwa akitoa ufafanuzi kuhusu taarifa iliyokuwa imetolewa na shirikisho la vyuo vikuu nchini humo,Tahliso.
Muungano huo unasema baada ya kuondoka afisi hizo,Bw Nondo alielekea chuoni na kuaga kuwa anaondoka kwenda nyumbani Madale.
"Ghafla katika hali ya kutatanisha, kuanzia saa 6 hadi saa 8 usiku alijitoa kwenye makundi yote ya mtandao wa kijamii wa WhatsApp jambo lililozua taharuki miongoni mwa watu wengi na kuanza kutaka kujua nini kimemsibu," muungano huo umesema kupitia taarifa.
"Saa 9.09 usiku alituma ujumbe mfupi kwa Mkurugenzi wa Idara ya Sheria TSNP Paul Kisabo ujumbe uliosomeka 'Am at risk!' (Nimo hatarini)."
Muungano huo umesema juhudi za kuwasiliana naye kwa simu kufikia sasa bado hazijafanikiwa na wamesema,wamepiga ripoti kwa jeshi la polisi katika kituo cha chuo kikuu cha Dar es Salaam.
Taarifa ya chama hicho cha wanafunzi imesema Bw.Nondo amekuwa akipokea vitisho kutoka kwa watu wasiojulikana ambapo hivi karibuni anadaiwa kukamatwa na askari wa jeshi la polisi eneo la Milimani City na kutuhumiwa kwamba "analeta uchochezi wa baadhi ya wanafunzi waliokosa mikopo ya elimu ya juu kuandamana."
"Mara kadhaa kumekwua na makundi ya watu asiowatambua na wenye nguo za kiraia wakijitambulisha kama watu wa usalama ambao wamekuwa wakimfuatilia na kumpa vitisho hivyo," taarifa hiyo inasema.
Muungano huo umesema viongozi mbalimbali wa TSNP wamekuwa wakipokea vitisho tofauti tofauti ambapo Muungano wa Mashirika ya Kutetea haki za kibinadamu Tanzania (THRDC) pia wametoa wito kwa polisi kufanya uchunguzi na kuhakikisha Bw. Nondo anapatikana akiwa salama.
"Kutoweka kwa Abdul huenda kunahusiana na kazi yake katika kutetea haki za kibinadamu," imesema taarifa iliyotolewa na mratibu wa kitaifa wa THRDC Onesmo Olengurumwa.

MATUKIO YA MAUAJI NA KUTOWEKA KWA WATU TANZANIA

§  Mauaji ya Kibiti mwaka 2017: Viongozi wa CCM, askari zaidi ya 10 na wananchi karibu 40 katika eneo la Kibiti walishambuliwa na kuuwawa na watu wasiojulikana.
§  11 Februari,2018 Kiongozi wa Chadema Daniel John alitekwa na kisha aliuwawa kikatili wakati wa Kampeni za Uchaguzi mdogo wa jimbo la Kinondoni.
§  Mnamo 7 Septemba,2017, Mnadhimu Mkuu wa upinzani bungeni, mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu alipigwa risasi na watu wasiojulikana katika eneo la Area D Mkoani Dodoma. Bw Lissu pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika.
§  21 Novemba,2017 Mwandishi wa habari wa Mwananchi Communications Limited Azory Gwanda alipotea katika mazingira ya kutatanisha na mpaka sasa hajapatikana.
§  Msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema Ben Saanane alipotea katika mazingira ya kutatanisha na mpaka sasa hajulikani alipo.
Habari zaidi ni P5TANZANIA LIMITED
Chanzo:bbc

Comments

Popular posts from this blog

HISTORIA FUPI YA ABDULRAHMAN KINANA ALIYEJUZULU UKATIBU MKUU CCM

FAHAMU HISTORIA YA JOKETI ALIYETUMBULIWA NA UVCCM

HISTORIA FUPI YA LAZARO NYALANDU ALIYEIBWAGA CCM NA KUHAMIA CHADEMA