MANISPAA YA MPANDA KUCHUKUA HATUA KUSURU KUFUNGWA MACHINJIO YA NG’OMBE-Septemba 4,2017
Na.Issack Gerald Bathromeo Mashama
Jengo la machinjio ya Mpanda Hotel Manispaa ya Mpanda |
Hatua hiyo imethibitishwa na
Mkurugenzi Mtendaji Manispaa ya Mpanda Bw.Michael Nzyungu amebainisha hatua
hiyo kufuatia Mamlaka ya Maji na usafi wa Mazingira Manispaa ya Mpansa (MUWASA)
kusema kuwa haina maji ya kutosha.
Nzyungu amesema makubaliano ya
uchimbaji wa kisima ili kunusuru hali ya ukosefu wa maji katika machinjio
umeafikiwa leo katika vikao vya ndani vya Manispaa ambapo hatua inayofuata ni
kutangaza zabuni ambapo matarajio ni kuanza kuchimbwa kisima hicho kwa
takribani wiki mbili zijazo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa mamlaka
ya maji na usafi wa mazingira Manispaa ya Mpanda Mhandisi Zacharia Nyanda
amesema tatizo la uhaba wa maji katika machinjio ya Mpanda Hotel inatokana na
kiasi kidogo cha maji kilichopo katika vyanzo.
Baadhi ya wafanyakazi wanaofanya kazi
katika machinjio ya Mpanda Hotel ambao hawakutaka kutaja majina yao kwa madai
kuwa wao siyo wasemaji,wamesema siku ya jana walishindwa kuchinja ng’ombe
kutokana na ukosefu wa maji ambapo wamesema tatizo hilo limekuwa likitokea
takribani mara nne kwa mwezi na kueleza kuwa tatizo hilo limekuwepo kwa muda
mrefu.
Kwa sasa machinjio ya Mpanda Hotel
yana matenki 3 ya maji yenye ujazo wa lita 12,500 ambapo kwa mjibu wa
Mkurugenzi wa Manispaa hata tenki la lita 2500 halijawahi kujaa maji tangu
huduma ya maji ianze kutolewa katika eneo hilo la machinjio.
Ng’ombe wapatao 50 huchinjwa kila
siku ambapo kila ng’ombe anayechinjwa hulipiwa shilingi 5000/=kama ushuru
ambapo hata hivyo machinjio hayo yatanatarijwa kuhamishwa kutoka eneo hilo
lililopo Mtaa na kata ya Mpanda Hotel baada ya kujenga machinjio makubwa nay a
kisasa nje kidogo kutoka katikati ya mji.
Mwaka 2015 Mamlaka ya Chakula na dawa
nchini TFDA ilifunga machinjio ya Mpanda Hotel kutokana na sababu mbalimbali
ikiwemo uchafu uliotokana na tatizo la ukosefu wa maji kwa kuwa uwepo wa uchafu
ulikuwa ukihatarisha afya za walaji.
Comments