KUMEKUCHA BUNGENI TENA ,MISWADA 6 UKIWEMO WA HABARI KUWASILISHWA,WABUNGE WA UPINZANI MGUU SAWA BUNGENI
Na.Issack Gerald
Bathromeo
MKUTANO wa Nne wa Bunge la 11 unatarajiwa kuanza leo mjini Dodoma,
huku miswada sita ukiwemo wa Sheria ya Upatikanaji wa Habari ukitarajiwa
kuchukua nafasi kubwa.
Katika mkutano huo, wabunge wa kambi ya upinzani ambao
walisusia siku kadhaa za mkutano uliopita, wamesema kwamba watahudhuria.
Mbunge wa Vunjo, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), alithibitisha
jana kwamba wabunge wa upinzani wataingia bungeni.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kitengo cha Habari, Elimu na
Mawasiliano ya Bunge kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana, jumla ya maswali
110 yanatarajiwa kuulizwa na wabunge na kujibiwa na Serikali.
Aidha, Waziri Mkuu anatarajiwa kuulizwa maswali 16 ya papo
kwa hapo. Taarifa hiyo ilisema miswada sita ya sheria iliyosomwa kwa mara ya
kwanza katika Mkutano wa Tatu wa Bunge na baadaye kupelekwa katika kamati
husika ili ifanyiwe kazi, itaendelea kushughulikiwa katika hatua zinazofuata
ikiwa ni pamoja na kusomwa kwa mara ya pili, kamati ya Bunge zima na kusomwa
kwa mara ya tatu.
Miswada hiyo ni pamoja na ule wa Sheria ya Upatikanaji wa
Habari ya mwaka 2015, Muswada wa Sheria ya Utathmini na Usajili wa Wathamini wa
mwaka 2016, Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serika wa
mwaka 2016.
Pia utakuwepo Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Wanataaluma
wa Kemia wa mwaka 2016, Muswada wa Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo wa
mwaka 2016 na Muswada wa Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi ya mwaka 2016.
Kufikia jana, mji wa Dodoma ulikuwa umefurika wageni mbalimbali
wakiwemo wabunge na maofisa wa serikali wanaohamia tayari kuanza kuendesha
shughuli zao katika makao makuu mapya ya Serikali, mjini humo.
Fuatilia zaidi kupitia P5TANZANIA.BLOGSPOT.COM
Comments