CHAMA CHA MADEREVA WAFANYAKAZI TANZANIA (TADWU) KUTOA TAMKO LEO KUHUSU MADEREVA NA WAAJIRI WAO
CHAMA
cha Madereva Wafanyakazi Tanzania (TADWU), kimesema madereva nchi nzima
watakuwa mapumziko kwa wiki moja au zaidi kwa ajili ya kujiunga na mafunzo ya
udereva.
Akizungumza
jana jijini Dar es Salaam, Katibu wa TADWU, Rashid Said, alisema baada ya
mazungumzo na Kamati ya Kudumu ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, wameshindwa
kuafikiana na kuona kuwa matajiri ndiyo wana nguvu zaidi kuliko wao waajiriwa.
Alisema
kutokana na hali hiyo wameamua kutoendelea na mgomo na badala yake kuanzia
Agosti 19 (Jumatano), hadi 24, mwaka huu watakuwa na mafunzo ya udereva nchi
nzima.
“Tumeona
suala la shinikizo la migomo halina matunda kwetu na kwa vile mazungumzo na
Serikali yamekwama, tumeamua kutumia mtindo mpya wa kupiga kwa kutumia bunduki
kubwa…tutaingia mafunzoni kwa wiki moja au zaidi madereva wote,” alisema Said.
Alisema
anaamini njia hiyo mpya itasaidia kupambana na maadui ambao ni waajiri wao
wanaowanyima haki zao za msingi.
“Kwa
kuwa hatujaridhika na maamuzi yaliyofikiwa katika kikao cha mwisho cha
upatanishi chini ya kamati ya Waziri Pinda, tumebaini hakuna urafiki wa kudumu
kati ya tajiri na masikini,” alisema.
Aliongeza
kuwa hawawezi kucheka na waajiri ikiwa yaliyopiganiwa hayajatekelezwa,
watahakikisha wanaendelea kupambana japokuwa wanaopambana nao ni vigogo.
“Sisi
kama chama tunafuata maelekezo ya wanasheria wetu ambao wamewaeleza wasigome
wafuate sheria na hawatagoma bali watakuwa na mafunzo nchi nzima,” alisema.
Alisema
mafunzo hayo yatafanyika kwa kanda nchi nzima, Pwani itakuwa ni Dar es Salaam,
Kaskazini Arusha na Kusini (Mtwara).
Pia
aliongeza madereva wote wa Kanda ya Ziwa watahudhuria mafunzo hayo Mwanza na
Kanda ya Juu, Mbeya hivyo wananchi wawe wavumilivu kipindi chote cha mafunzo
kwa kuwa yanalenga kuokoa maisha yao katika kupunguza ajali.
Said
alisisitiza kuwa madereva wameburuzwa na kunyanyaswa vya kutosha na waajiri wao
hivyo sasa ni muda wa ukombozi kwa kusikilizwa matakwa yao kwa kuwa mgogoro
uliopo kati ya madereva na wamiliki ni mkubwa.
Comments