WAGOMA KUSHIRIKI SHUGHULI ZA MAENDELEO MPAKA WASOMEWE MAPATO NA MATUMIZI
NA.Issack Gerald-Nsimbo Katavi
Wakazi wa kijiji cha Magamba
kilichopo kata ya Magamba Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo Mkoani Katavi wamesema
hawatashiriki shughuli mbalimbali za maendeleo zikiwemo za ufyatuaji tofali za kijiji ikiwa
hawatasomewa taarifa ya mapato na matumizi iliyo sahihi.
Wakazi kijiji hao wakizungumza na P5 TANZANIA Kijijini hapo wamesema
taarifa ambazo wamekuwa wakisomewa na uongozi wa kijiji chao hazina ukweli
ukilinganisha na kile wanachokichangia na kuongeza kuwa mkutano wa mwisho
uliofanyika mwezi wa sita ulivurugika kufuatia kutokuwepo maelewano kati ya viongozi na
wakazi baada ya taarifa zilizokuwa zikitolewa kutokuwa sahihi.
Kwa upande wake mwenyekiti wa kijiji cha Magamba Anna
Thomas amesema wanatarajia kuitisha mkutano wa dharura kusoma taarifa ya mapato
na matumizi kuanzia mwaka 2013 hadi 2014 ili kuondoa utata uliopo.
Hata hivyo pamoja na mambo mengine
Afisa Mtendaji Kata ya Magamba George Iresha amesema kuna changamoto ya
maandalizi ya mapato na matumizi katika vijiji vilivyo katika kata ya magamba kutokana
na kutokuwepo wa maafisa watendaji wa vijiji ambao kimsingi ndio wanaotakiwa
kuandaa taarifa hizo.
Suala la kutosoma mapato na matumizi
katika serikali za mitaa limekuwa likiibuka katika vijiji na mitaa mingi Mkoani
Katavi na kusababisha mgogoro kati ya uongozi na wananchi.
Kwa mjibu wa taratibu za mamlaka za
serikali za mitaa hapa nchini ,mapato na matumizi yanatakiwa kusomwa kila baada
ya miezi mitatu.
Comments